24.9 C
New York

Dc Temeke avitaka vyombo vya dola kuchunguza showroom za magari

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MKUU wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi katika showroom za magari wilayani humo ili kubaini kama baadhi yake zinatumika kutakatisha fedha zinazotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Mapunda amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuvunja mtandao wa kifedha unaowezesha biashara ya dawa za kulevya kuendelea kushamiri, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa hizo hayawezi kuishia kwa kuwakamata watumiaji na wasafirishaji pekee, bali yanapaswa kulenga pia vyanzo vya fedha vinavyoendesha biashara hiyo.

Akizungumza Julai 23, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa tamasha la “Kataa Dawa za Kulevya, Timiza Malengo Yako” lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), alisema dawa za kulevya ni tishio kwa maendeleo ya taifa kwa kuwa huharibu nguvu kazi, huongeza uhalifu na kudhoofisha uchumi wa nchi.

“Tatizo la dawa za kulevya ni mtambuka na haliwezi kutatuliwa na taasisi moja pekee. Linahitaji ushirikiano wa wananchi wote ili kupunguza matumizi na biashara ya dawa hizo nchini,” amesema Mapunda.

Amewataka wananchi, hususan vijana, kushiriki kikamilifu katika mapambano hayo kwa kutoa taarifa za wahusika, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kuelimisha wengine kuhusu madhara yake.

Pia aliwaonya vijana dhidi ya kuvutiwa na maisha ya kifahari yasiyo na maelezo ya wazi, akisema baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya hutumia utajiri huo kuwashawishi vijana kuingia katika biashara hiyo haramu.

Mapunda aliwataka wakazi wa Temeke kutumia namba maalumu za mamlaka husika kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kushirikiana na Serikali katika kulinda afya ya jamii na mustakabali wa taifa.

Aidha, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama wilaani humo kuendelea kufuatilia watu wanaoonyesha utajiri usioendana na kipato chao ili kubaini iwapo fedha wanazotumia zinatokana na biashara haramu.

Alisema njia endelevu ya kupunguza tatizo hilo ni kukata mnyororo wa usambazaji wa dawa za kulevya sambamba na kuwekeza katika elimu kwa watoto, vijana na wazazi kuhusu madhara ya matumizi ya dawa hizo.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Kinga na Tiba wa DCEA, Dk. Cassian Nyandindi, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa kuhusu wauzaji na wasambazaji pamoja na kuelimisha jamii ili kuzuia watu kuingia kwenye matumizi ya dawa hizo.

Amesema waraibu wa dawa za kulevya wanapaswa kupelekwa katika vituo vya tiba na utengamao ili wapate huduma stahiki na kurejea katika maisha ya kawaida, akisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni nguzo muhimu ya mafanikio ya mapambano hayo.

Dk. Nyandindi alisema Mkoa wa Dar es Salaam unaendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayoathiriwa zaidi na dawa za kulevya, huku kampeni ya mwaka huu ikianzia Temeke kutokana na ukubwa wa tatizo hilo.

“Katika Kituo cha Metadoni cha Temeke pekee, watu 2,500 wamesajiliwa na wanaendelea kupatiwa matibabu ya uraibu wa heroin kupitia dawa ya methadone,” amesema.

Ameongeza kuwa tangu mwaka 2022 zaidi ya watu 14,000 wamepata huduma katika kitengo cha afya ya akili cha Temeke kutokana na athari za uraibu wa dawa za kulevya.

Dk. Nyandindi amesema DCEA itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kukamata wahalifu, kutoa elimu kwa umma, kuimarisha huduma za tiba na utengamao pamoja na kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kudhibiti biashara hiyo.

Amewahimiza wazazi kuanza mapema kuzungumza na watoto wao kuhusu madhara ya dawa za kulevya ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, akisisitiza kuwa kinga ndiyo njia bora ya kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya janga hilo.

Related articles

Recent articles