Na Esther Mnyika, GAZETINI
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya mabadiliko ya ratiba ya uendeshaji wa Upimaji na Mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026, kufuatia utabiri wa uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya El Niño katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.
Kutokana na mabadiliko hayo, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili, Darasa la Nne na Kidato cha Pili utafanyika mwezi Oktoba 2026, huku Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ukianza Oktoba na kukamilika mapema Novemba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, Septemba 25, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Wizara kuzingatia uwezekano wa mvua kubwa kutokea mwezi Novemba 2026 na athari zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa mitihani.
Amesema mabadiliko hayo yanalenga kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa, hususan mafuriko, changamoto za usafiri, kukatika kwa umeme na kuathirika kwa mawasiliano, hali ambazo zinaweza kuvuruga uendeshaji wa mitihani pamoja na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na wasimamizi.
“Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya utabiri iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tarehe 18 Agosti 2026, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa hali ya El Niño, ambayo inatarajiwa kuathiri mvua za Vuli katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026 na kuendelea hadi Januari 2027,” amesema.
Naibu Waziri amesema lengo jingine la marekebisho hayo ni kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine wanaohusika katika uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka zake dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa.
Ratiba mpya ya upimaji na mitihani
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026, badala ya Oktoba 21 na 22 kama ilivyopangwa awali.
Amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili, ambao awali ulipangwa kufanyika Novemba 17 na 18, sasa utafanyika Oktoba 7 na 8, 2026.
Kwa upande wa Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, Profesa Mohamed amesema upimaji huo ambao awali ulipangwa kufanyika kuanzia Novemba 2 hadi 13, sasa utafanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23, 2026.
Aidha, Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ambao awali ulipangwa kuanza Novemba 9 hadi 27, sasa utaanza Oktoba 19 na kukamilika Novemba 6, 2026.
Wizara imesisitiza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuhakikisha upimaji na mitihani ya taifa inafanyika katika mazingira salama na yenye ufanisi, huku ikizingatia tahadhari zinazoweza kuchukuliwa kutokana na utabiri wa hali ya hewa kwa kipindi husika.


