26 C
New York

WHO yaanza majaribio ya dawa ya kuzuia maambukizi ya ebola

Published:

DRC, Congo

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuanza kwa majaribio ya kwanza ya kitabibu ya dawa inayolenga kuzuia maambukizi ya Ebola kwa watu waliokaribiana na wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.

Majaribio hayo, yanayojulikana kwa jina la EBO PEP, yanalenga kutathmini uwezo wa dawa ya obeldesivir kuzuia maambukizi ya aina ya Bundibugyo Ebola kwa watu waliowahi kukutana na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo.

Kwa mujibu wa WHO, dawa hiyo ya majaribio, inayotengenezwa na kampuni ya Marekani ya Gilead Sciences, hutumiwa kwa njia ya kumeza na tayari imeonyesha matokeo ya kutia matumaini katika tafiti za awali.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuanza kwa majaribio hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha juhudi za kimataifa za kuzuia maambukizi ya Ebola.

“Kila mafanikio huanza na matumaini. Ikiwa dawa hii itathibitika kuwa na ufanisi kwa watu walio katika hatari kubwa baada ya kuathiriwa, inaweza kuwa hatua kubwa mbele katika kuzuia maambukizi ya Ebola,” amesema Tedros.

WHO imeeleza kuwa endapo majaribio hayo yataonyesha mafanikio, dawa hiyo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuwalinda wahudumu wa afya, wanafamilia na watu wengine waliokaribiana na wagonjwa wakati wa milipuko ya Ebola, hatua itakayosaidia kupunguza kasi ya maambukizi na kuimarisha udhibiti wa ugonjwa huo.

Related articles

Recent articles