MIAMI, Marekani
WAKATI huu fainali za Kombe la Dunia zikiendelea, baadhi ya wanasoka wenye majina makubwa wametangaza kustaafu muda mfupi tu baada ya timu zao za taifa kutolewa.
Je, ni nani na nani waliotundika daluga kuzitumikia timu zao za taifa hata kabla ya kumalizika kwa michuano hiyo inayofanyika Marekani, Canada na Mexico? Endelea kusoma …
CRISTIANO RONALDO
Miongoni mwao ni nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Ureno, ambaye ‘chama’ lake liling’olewa baada ya kufungwa bao 1-0 na Hispania.
Ronaldo alianza kucheza Kombe la Dunia akiwa na umri wa miaka 21 na hizi ni fainali zake za sita, safari hii akiwa mchezaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi (miaka 41).
Licha ya kustaafu timu ya taifa akiwa hajaipa Kombe la Dunia, staa huyo wa Al-Nassr ya Saudi Arabia amesema hana cha kujutia. “Mungu amekuwa mwema sana kwangu. Amenipa kila kitu. Amenipa mafanikio ambayo sikuwahi kuyatarajia,” alisema.
NEYMAR
Mfungaji bora wa muda wote wa timu ya soka ya Taifa ya Brazil. Alitangaza kustaafu kuitumikia baada ya kutolewa Kombe la Dunia kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Norway ya Erling Haaland.
Neymar (34), alianza kuitumikia Brazil mwaka 2010 lakini majeraha ya mara kwa mara yamemzuia kufanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni.
Katika ujumbe wake wa kuwaaga mashabiki wa Brazil, mshambuliaji huyo wa Santos alisema: “Nimepambana vya kutosha.”
OCHOA
Kipa wa Mexico. Akiwa na umri wa miaka 40, mchezaji wa tatu mwenye umri mkubwa zaidi msimu huu, amestaafu majukumu ya timu ya taifa.
Ochoa alitangaza uamuzi wake huo baada tu ya Mexico kutolewa na England katika hatua ya 16 Bora. Walifungwa mabao 3-2.
“Nimefurahia kila hatua (nikiwa na Mexico). Nilijitoa kwa moyo wote. Naondoka nikiwa najivunia kupata uzoefu huu,” alisema Ochoa.
MANUEL NEUER
Alishastaafu kuitumikia Ujerumani, kabla ya kurudi langoni kwa ajili ya fainali za mwaka huu. Neuer amestaafu tena akiwa na umri wa miaka 40.
Ujerumani haikuwa na mwenendo mzuri safari hii, ambapo safari yao iliishia hatua ya 32 Bora baada ya kufungwa na Paraguay.
“Licha ya kumaliza vibaya, sijutii kurudi,” alisema kipa huyo na kusisitiza kuwa alirejea kikosini ili kuwapa morali wachezaji chipukizi.
RIYARD MAHREZ
Safari ya Algeria msimu huu wa Kombe la Dunia iliishia hatua ya 32 Bora. Walitolewa kwa kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Uswis.
Ni baada tu ya mechi hiyo, Mahrez ambaye ndiye nahodha wa kikosi, alitangaza kuachana na timu ya taifa.
Mahrez (39), ameeleza kuwa uamuzi wake huo umelenga kuwapa wachezaji chipukizi nafasi ya kuitumikia timu yao ya taifa.


