24.1 C
New York

Wachambuzi wa soka wanaolipwa zaidi EPL

Published:

LONDON, Uingereza

SOKA limekuwa likitoa fursa nyingi. Mathalan, ndani ya klabu, limeajiri viongozi, wachezaji, makocha, madaktari, wapishi, na wafanyakazi wengine.

Kwa miaka mingi, limekuwapo kundi la wachambuzi wa soka, ambalo pia limekuwa likinufaika vilivyo na uwepo wa mchezo huo.

Makala haya yanakuletea wachambuzi wa Ligi Kuu ya England (EPL), wanaotajwa kuwa ndiyo wanaolipwa fedha nyingi zaidi.

GARY NEVILLE

Ni beki wa zamani wa Manchester United na timu ya Taifa ya England. Ni mchambuzi wa kituo cha televisheni cha Sky Sports, ambapo amekuwa akilipwa Pauni 1,100,000 (zaidi ya Sh bil. 3.8 za Tanzania) kwa mwaka.

JAMIE CARRAGHER

Lejendari wa Liverpool na timu ya Taifa ya England. Mbali ya Sky Sports, pia ni mchambuzi wa kituo kingine cha televisheni cha CBS Sports. Kazi hiyo inamuingizia Pauni 1,000,000 (zaidi ya Sh bil. 3.5) kwa mwaka.

ALAN SHEARER

Huyo ndiye mfungaji bora wa muda wote wa EPL. Amekuwa akichambua soka kupitia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Kazi hiyo inampa mshahara wa Pauni 440,000 (zaidi ya Sh bil. 1.5) kila mwaka.

WAYNE ROONEY

Licha ya kujihusisha na ukocha, pia straika huyo wa zamani wa Man United amekuwa akifanya uchambuzi wa soka. BBC inamlipa Rooney mshahara mnono wa Pauni 400,000 (zaidi ya Sh bil. 1.4) kila mwaka.

MARK CHAPMAN

Mchambuzi ambaye pia ni mtangazaji wa BBC akipeana zamu na Gabby Logan, Alex Scott na Jason Mohammad. Mshahara wake ni Pauni 325,000 (zaidi ya Sh bil. 1.1 za Tanzania).

Related articles

Recent articles