MEXICO CITY, Mexico
UWANJA wa Azteca unaopatikana Kusini mwa Mji Mkuu wa Mexico, Mexico City. Ni moja ya viwanja vya soka vyenye historia ya aina yake.
Baada ya Mexico kushinda zabuni ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 1970, muhandisi Pedro Ramirez Vazquez alipewa jukumu la kujenga uwanja wenye uwezo wa kupokea mashabiki zaidi ya 100,000.
Vazquez alitakiwa kujenga uwanja wenye hadhi ya Maracana, ambao majirani zao, Brazil, walitumia wakiwa wenyeji wa fainali za mwaka 1950.
Chini ya injinia huyo, Uwanja wa Azteca ukajengwa baada ya miamba yenye uzito wa kilogramu milioni 180 kufukuliwa ardhini.
Kwa mara ya kwanza, Uwanja huo ukatumika kwa mechi ya soka ya kimataifa wakati wa michuano ya Olimipiki ya mwaka 1968.
Hadi sasa, Azteca unabaki kuwa ndiyo uwanja pekee katika historia ya soka kuandaa misimu mitatu tofauti ya Kombe la Dunia (1970, 1986 na 2026).
Mbali na hilo, ni Uwanja uliobeba maajabu mengi, ukitosha kuingia kwenye historia ya Kombe la Dunia na mchezo wa kandanda kwa ujumla.
Mosi, ni katika dimba hilo, ulichezwa mchezo wa kihistoria wa nusu fainali ya Kombe la Dunia kati ya Ujerumani Magharibi na Italia.
Maajabu ya mchezo huo ni kwamba baada ya dakika 90, timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1 lakini zile 30 za nyongeza zilishuhudia mabao matano yakifungwa. Italia ilishinda 4-3.
Pili, ni katika Uwanja huo pia, Brazil ilitwaa ubingwa msimu huo kwa ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mexico. Bao la mwisho la Brazil lilifungwa na Roberto Carlos baada ya wachezaji watatu tu kugusa mpira.
Tatu, ni katika Uwanja huo, Diego Maradona wa Argentina alifunga bao la mkono wakati Mexico ikiwa tena mwenyeji miaka sita baadaye.
Tukio hilo la kusisimua lilitokea katika robo fainali yao dhidi ya England. Dakika nne baadaye, alitumia sekunde 11 kuwapita wachezaji watano wa England akitokea katikati ya uwanja, kisha kumzunguka kipa wao na kufunga bao la pili.
Nne, nje ya soka, Uwanja huo umekuwa ukitumika kwa michezo mingine, na hata shoo za burudani.
Mwaka 1993, bondia raia wa Mexico, Julio Cesar Chavez, alikuwa hapo na kutetea ubingwa wa WBC kwa kumtwanga Greg Hauger.
Mwaka huo huo, Mfalme wa muziki wa Pop, Michael Jackson (sasa marehemu), alifanya shoo kali katika ziara yake ya ‘Dangerous World Tour’.
Pia, mwaka 1999, ibada kubwa iliyoongozwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki wakati huo, Papa John Paul II, ilifanyika katika Uwanja huo.
Baada ya marekebisho kadhaa, Uwanja huo kwa sasa unapokea mashabiki 87,500 na klabu za Ligi Kuu ya Mexico, Club America na Cruz Azul, zimekuwa zikiutumia kwa mechi zake za nyumbani.


