Na Hassan Mwasha
DAKIKA 90 tu za mchezo kati ya Fountain Gate na Singida Black Stars ndizo zilizopeperusha ndoto ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-26.
Kabla ya mechi za mwisho wa msimu kuchezwa jana Juni 30, 2026, Fei Toto wa Azam ndiye aliyekuwa kinara kwa mabao 15, akifuatiwa na Allan Okello (Yanga) na Mossi Ndumumwe (Singida Black Stars), kila mmoja akiwa amepasia nyavu mara 14.
Hata hivyo, si Fei Toto wala Okello aliyeongeza bao, bali ni Ndumumwe ndiye aliyepachika ‘hat-trick’ dhidi ya Fountain Gate na kubeba kiatu akiwa na mabao 17.
Kwa upande mmoja, ni maumivu kwa Fei Toto, ikizingatiwa kuwa kiungo mshambuliaji huyo alikuwa kinara wa mabao kwa sehemu kubwa ya msimu uliomalizika.
Kwa upande mwingine, Ndumumwe raia wa Burundi ameendeleza ubabe wa wachezaji wa kigeni kwenye tuzo hiyo ya kuzifumania nyavu.
Iko hivi; msimu uliopita, 2024-25, kiatu kilitua kwa aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba raia wa Ivory Coast, Jean Ahoua, kwa mabao yake 16.
Aidha, msimu wa nyuma yake, kwa maana ya 2023-24, tuzo ya mfungaji bora wa Ligi ilinyakuliwa na kiungo raia wa Burkina Faso, Stephanie Aziz Ki, ambaye alifunga mabao 21.
Ni msimu ambao Fei Toto pia alikaribia kuchukua lakini alizidiwa kete siku ya mwisho na kushika nafasi ya pili akiwa na mabao 19.
Pia, katika msimu wa 2022-23, tuzo hiyo ya mfungaji bora wa Ligi iliangukia mikononi mwa mchezaji mwingine wa kigeni, Fiston Mayele.
Mshambuliaji huyo wa kati wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) alimaliza msimu akiwa ameifungia Yanga mabao 15.
Kwa ufupi, mara ya mwisho kwa mchezaji mzawa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu wa 2021-22. Ni George Mpole.
Akiwa kinara wa safu ya ushambuliaji ya Geita Gold, alimaliza msimu huo akiwa amefunga mabao 17, akimzidi moja Mayele aliyeshika nafasi ya pili.
Itakumbukwa kuwa vita ya Mpole na Mayele iliamuliwa siku ya mwisho ya msimu, kama ilivyotokea kwa Fei Toto, Okello na Ndumumwe.


