MIAMI, Marekani
WAKATI huu fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026) zikiendelea, moja ya vipaumbele katika nchi wenyeji – Marekani, Mexico na Canada – ni suala la usalama.
Kwa nchini Marekani, ndege zisizo na rubani (drones) zaidi ya 1,000 zimebainika kuzengea kwenye maeneo mbalimbali yanayohusika moja kwa moja na michuano hiyo, vikiwamo viwanja.
Taarifa hiyo inakuja wakati huu Marekani ikiwa kwenye ‘uadui’ na mataifa kadhaa, hasa mgogoro wake na Iran, achilia mbali magaidi wa Hezbollah nchini Lebanon.
Sasa, kwa mujibu wa taarifa, ndege zisizo na rubani, ambazo hazijafahamika zilitumwa na nani, zimeripotiwa kunaswa na rada za Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) kwa kushirikiana na Kituo cha Polisi wa Kimataifa (IPCC).
Taarifa zinaeleza zaidi, kwamba FBI imekamata ndege zaidi ya 500, kwa mujibu wa Doug Olson, ambaye ni ofisa maalumu wa Shirika hilo anayehusika na uratibu wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Tangu kuanza kwa michuano hiyo Juni 11, 2026, Serikali ya Marekani imesambaza polisi wake katika miji yote 11 inayotumika kwa mechi.
Aidha, polisi hao ‘walimwagwa’ baada ya mafunzo maalumu waliyopatiwa katika kituo cha FBI.
Wiki chache zilizopita, kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia, FBI ilinasa taarifa za mapema na kudhibiti shambulizi la kigaidi lililopangwa kufanyika katika ‘birthday’ ya Rais Donald Trump ya kutimiza umri wa miaka 80.
FBI ilibaini kuwa shambulizi hilo lingetekelezwa kwa kutumia ndege zisizo na rubani zilizotengezwa kwa teknolojia ya hali ya juu. Wahusika hawakufahamika.
Wakati wa michuano ya Olimipiki ya mwaka 2024 jijini Paris, mamlaka za Ufaransa zilinasa uwepo wa drone zaidi ya 350 na kufanikiwa kukamata 81.


