LOS ANGELES, Marekani
BINADAMU wa kwanza kuwa trilionea, Elon Musk, alisherehekea kutimiza umri wa miaka 56 jana Juni 28, 2026.
Mbali ya kusherehekea kutimiza umri huo, pia ilikuwa ni furaha kwake kuona amemaliza kesi na bibiye aliyewahi kuwa naye kwenye mahusiano, Grimes.
Musk na mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 38, walikuwa kwenye mahusiano kwa miaka minne, kabla ya kuachana mwaka 2022.
Tangu walipoachana, Musk na Grimes waliingia kwenye uhusiano mbaya, ikiwamo kufikishana mahakamani.
Msingi wa kesi ni malezi ya watoto wao watatu – X Æ A-12 wa miaka sita, Exa Dark Sideræl Musk (4), Techno Mechanicus (4) – kabla ya kufikia makubaliano mwaka 2024.
Uhusiano wao ulianza kuwa kwenye vyombo vya habari mwaka 2018. Kwa miaka minne ya uhusiano, waliachana na kurudiana mara kadhaa.
Mwaka 2020, bibiye Grimes alitangaza kuwa na ujauzito wa tajiri huyo. Septemba, 2021, Musk alitangaza kuwa wameachana.
Lakini, alisema bado wanawasiliana kwa karibu. “Bado tunapendana, tunaonana mara kwa mara, hatuna shida,” alisisitiza.
Haikuchukua muda, wakarudiana. Machi, 2022, Grimes alitangaza wamepata mtoto wao wa pili aliyetokana na mimba ya mwanamke mwingine aliyepandikizwa mbegu za Musk.
“Naweza kusema ni mpenzi wangu, ingawa tuko mbali. Tunaishi nyumba tofauti lakini tunaonana mara kwa mara. Sitarajii watu kutuelewa,” alisema Grimes.
Septemba, 2023, wawili hao waliibuka kwa mara nyingine na kutangaza kupata mtoto wao wa tatu.
Baada ya mtoto huyo, haikuchukua muda mrefu, Grimes akafungua kesi mahakamani akitaka kupewa haki ya malezi ya watoto.
Kwa mujibu wake, Musk alikuwa akimuweka mbali na watoto kwa kumzuia kuwaona, kuwasiliana, na kuwa nao karibu.
Baada ya miaka mingi ya kuvutana, hatimaye kesi hiyo ilimalizika mwaka 2024 kwa Mahakama kuamuru Musk ampe ‘ex’ wake haki ya kujenga na kuimarisha uhusiano na watoto.


