Na Hassan Mwasha, Gazetini
MSIMU huu wa 2025-26 wa Ligi Kuu Bara utafikia ukomo wake kesho Juni 30,2026, kwa timu zote 16 kushuka dimbani.
Kwamba viwanja nane vitawaka moto kwa mechi za kufunga msimu na zote zitachezwa muda wote; saa 10 jioni.
Wenyeji wa Uwanja wa Jenerali Isamhuyo, JKT, watawakaribisha mabingwa watetezi, Yanga, wakati mchezo mwingine utakuwa kati ya Simba na KMC.
Aidha, Coastal Union watakuwa mbele ya mashabiki wao katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa mchezo dhidi ya Pamba Jiji ya Mwanza.
Huko mkoani Singida, nako kutawaka moto kwa dakika 90 za mechi kati ya wenyeji Fountain Gate na ‘ndugu’ zao, Singida Black Stars.
Kama hiyo haitoshi, jijini Mbeya nako ‘kitawaka’ kati ya wenyeji Mbeya City na timu tishio msimu huu kutoka mjini Tabora, TRA United.
Wakati huo huo, Mashujaa FC ya Kigoma itakuwa mbele ya mashabiki wake kuikaribisha timu kongwe ya mkoani Mbeya, Tanzania Prisons ‘Wajelajela’.
Siku hiyo pia, matajiri wa Chamazi, Azam FC, watakuwa nyumbani Azam Complex kumenyana na Dodoma Jiji, wakati Namungo watawakaribisha wakongwe wa soka la Morogoro, Mtibwa Sugar.


