MIAMI, Marekani
TEKNOLOJIA ya kumsaidia mwamuzi kwa marudio ya video (VAR) imeibua sintofahamu kwa baadhi ya maamuzi yake wakati huu wa fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea.
Moja ya maamuzi ya kushangaza ya VAR ni pale ilipolikataa bao halali la nyota wa Iran, Shoja Khalilzadeh, katika sare ya 1-1 dhidi ya Misri kwenye Uwanja wa Seattle.
Ni bao ambalo lingeipeleka Iran katika hatua ya 32 Bora, hivyo kukataliwa kwake kukaifanya timu hiyo kuishia makundi.
Katika tukio jingine, uamuzi wa VAR uliinyima penalti timu ya soka ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’ katika mchezo wao dhidi ya England uliomalizika kwa suluhu (0-0).
Dakika ya 79 ya mchezo huo uliochezwa mjini Boston, nyota wa England, Ezri Konsa, alimdondosha Prince Kwabena Adu kwenye boksi.
Baada ya mechi, kocha wa kimataifa wa Ureno anayeinoa Ghana, Carlo Queiroz, alitania akisema: “VAR ilikwenda kunywa kahawa.”
Aidha, lipo tukio jingine la mshambuliaji wa Brazil, Vinicius Jr, kunyimwa bao halali katika mchezo wao dhidi ya Scotland.
Katika dakika ya 22, VAR ilitafsiri kimakosa, kwamba staa huyo wa Real Madrid alimchezea rafu beki Jack Hendry na kuchukua mpira, kisha kufunga bao. Brazil ilishinda 3-0.
VAR ‘ilizungua’ tena katika mchezo ambao Ujerumani ilichezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ecuador. Bao la nyota wa Ujerumani, Leroy Sane, ndilo lililozua utata.
Kabla ya mpira kufika kwa Sane, tayari kulikuwa na faulo baada ya Aleksandar Pavlovic wa Ujerumani kumpandishia mguu Pedro Vite lakini VAR iliacha mambo yaende.


