LAGOS, Nigeria
LICHA ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuipa onyo, Serikali ya Nigeria imepiga hatua moja mbele katika mpango wake wa kukopa kiasi cha Dola bilioni tano kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Nigeria imepanga kuelekeza fedha hizo katika bajeti yake ya Mwaka 2026, ikilenga kufadhili baadhi ya miradi ya miundombinu.
Hata hivyo, IMF iliionya Nigeria kuhusu mkopo huo, ikieleza wasiwasi wake juu ya athari zake katika uchumi wa nchi hiyo ya Afrika ya Magharibi.
Onyo la IMF limekuja wakati tayari Nigeria imetajwa kuchota Dola bilioni 1.5 kati ya Dola bilioni tano walizokubaliana na UAE mwanzoni mwa mwaka 2026.
Machi 31, 2026, Bunge la Nigeria liliidhinisha mkopo huo, likisema makubaliano yaliyoingiwa na UAE hayana madhara yoyote kwa uchumi wa Taifa hilo.
Kwa upande wake, IMF imeeleza kuwa mkopo huo ni mzigo mwingine mzito kwa Nigeria, ikizingatiwa kuwa tayari ina deni la nje la Dola bilioni 51.9 kufikia Desemba 31, 2025.


