LOS ANGELES, Marekani
UMARURU wake ulianza mwaka 2008 baada ya kutumika kama mrembo wa video katika ngoma ya rapa Young Jeezy iitwayo ‘Put On’.
Ni wimbo ambao mbali ya Amber kuwa ‘video vixen’, ameshirikishwa pia Kanye West, hivyo rapa huyo naye akawepo siku ya kurekodi video.
Kuanzia hapo, Amber akaanza ukaribu na Kanye na mwishowe ukazaliwa uhusiano wa kimapenzi kati yao.
Amber akawa mkubwa ghafla, ikawa ni pamoja na kupata dili za matangazo katika kampuni za Louis Vuitton na kusaini mkataba wa Ford Models.
Kwa upande wake, akajitengenezea jina kama video vixen maarufu zaidi katika ngoma za muziki wa Hip hop.
Baadhi ya marapa waliompa kazi ni pamoja na Ludacris kupitia wimbo ‘What Them Girls Like’, Nicki Minaj kupitia ‘Massive Attack’ na Fabolous katika wimbo ‘You Be Killin’ Em’.
Haikushangaza kuona hata asilimia kubwa ya wanaume aliotoka nao ni mastaa wa muziki huo wa kufokafoka.
Ndiyo, alipoachana na Kanye mwaka 2010, Amber alianguka kwa rapa mwingine mkali, Wiz Khalifa, ambaye alifunga naye ndoa mwaka 2013 na kuachana 2014 wakiwa na mtoto mmoja wa kiume.
Baada ya kuachika, Amber alianza kuonekana na rapa mwingine, Machine Gun Kelly, kabla ya kuanza kutoka na staa wa Ligi Kuu ya Kikapu ya Marekani (NBA), Terrence Ross, mwaka 2016.
Mwanzoni mwa mwaka 2017, alihamia kwa supastaa wa Hip hop, 21 Savage, lakini kapo yao iliota mbawa miezi michache tu baadaye.
Mwaka 2019, alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram, kwamba anatarajia kupata mtoto akiwa na bosi wa lebo maarufu ya Def Jam, Alexander Edwards A.E.’
Mwaka 2009, Amber aliwashitua mashabiki wake aliposema: “Naweza kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanamke na naweza kuwa na mwanaume,” alisema.
Wakati fulani, Amber aliwahi kujitosa kwenye muziki na kuachia ngoma kadhaa, zikiwamo ‘Fame’ (ft. Wiz Khalifa) na ‘Loaded’.
Amber alizaliwa Oktoba 21, 1983, huko Philadelphia. Baba ni raia wa Ireland mwenye asili ya Italia, wakati mama anatokea Cape Verde.
Kutokana na ugumu wa maisha, hasa baada ya mama kuachana na wanaume wawili, akiwamo baba yake Amber, binti huyo alianza kazi chafu ya kucheza utupu kwenye klabu za starehe akiwa na umri wa miaka 15 tu.
Katika moja ya mahojiano yake, Amber alisema wakati huo alijaribu hata kuuza dawa za kulevya aina ya cocaine lakini aliacha kwa hofu ya kukamatwa.


