19.4 C
New York

Maisha, utata wa kifo, maziko ya Rais Edgar Lungu (1)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

HATIMAYE Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini imeitangazia ushindi familia ya Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, katika rufaa yake dhidi ya hukumu ya awali.

Agosti, 2025, Mahakama hiyo iliipa Serikali ya Zambia ushindi wa kumzika Lungu, hatua ambayo ilipingwa na familia kwa kukata rufaa.

Familia ilisema inapaswa kupewa haki ya kumzika mwanasiasa huyo aliyefariki Juni, 2025, pasi na kufuata taratibu za Serikali ya Zambia.

Hata hivyo, licha ya sasa familia kushinda ombi la kutaka Lungu azikwe Afrika Kusini, bado Serikali ya Zambia ina nafasi ya kukata rufaa.

Ni kwa takribani mwaka mmoja sasa, familia ya Lungu na Serikali ya Zambia wamekuwa kwenye mvutano juu ya ni upande upi utamzika kiongozi huyo.

Serikali inashikilia msimamo wake wa kufuata taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kumzika katika makaburi ya wastaafu wengine jijini Lusaka.

Hatua ya familia kung’ang’ania kumzika Lungu inakuja wakati pia ikidai kwamba alisema hataki mwili wake uwe karibu na Rais wa sasa, Hakainde Hichilema, endapo ingetokea akafariki.

Lungu, ambaye aliiongoza Zambia kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, alifariki akiwa na umri wa miaka 68 wakati akiendelea na matibabu mjini Pretoria, Afrika Kusini.

GAZETINI kupitia vyanzo mbalimbali vya habari, inakuletea mfululizo wa makala juu ya safari ya maisha, mikasa ya kisiasa, kifo na hata utata unaoendelea juu ya maziko ya mwanasiasa huyo mkongwe wa Chama cha Patriotic Front (PF).

Tuanzie hapa; Lungu alizaliwa Novemba 11, 1956 katika Hospitali ya Ndola Central. Alipohitimu Shahada ya Sheria mwaka 1981 katika Chuo Kikuu cha Zambia, aliajiriwa katika Kampuni ya Andrea Masiye and Company mjini Lusaka.

Alijitosa katika siasa mwaka 1996, alipowania ubunge wa Jimbo la Chawama akiwa mgombea binafsi (asiye na chama). Hakushinda, na badala yake alizidiwa kura na mgombea wa Chama cha MMD, Christon Tembo.

Chama cha United Party for National Development kilipoanzishwa mwaka 1998, Lungu alijiunga nacho.

Mwaka 2001, alijiunga na Chama kipya wakati huo, Patriotic Front (PF), na kugombea tena ubunge katika Jimbo la Chawama. Safari hii, alianguka zaidi akishika nafasi ya saba kwa asilimia 2.43 ya kura.

Katika Uchaguzi wa 2011, alijitosa tena kwenye Jimbo hilo hilo na kushinda kiti cha kuingia Bungeni kupitia Patriotic Front.

Ndipo Lungu alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kabla ya kupanda hadi Waziri wa Mambo ya Ndani (2012) na Waziri wa Ulinzi (2013).

Ndani ya Chama chake, Patriotic Front, Lungu pia alishika nafasi mbalimbali kwa nyakati tofauti, zikiwamo Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Nidhamu na Katibu Mkuu.

Kuanzia mwaka 2013 hadi 2014, Lungu aliiongoza Zambia akitokea Ikulu baada ya Rais wa wakati huo, Michael Sata, kusumbuliwa na maradhi ya muda mrefu yaliyomlazimisha kufuata matibabu nje ya nchi.

Hatimaye, Sata alifariki Oktoba 28, 2014, hivyo Makamu wa Rais, Dkt. Guy Scott, kukaimu kiti chake cha urais ili kusubiri uchaguzi mdogo.

Hapo, Lungu alionekana kuwa ndiye mwenye nafasi kubwa ya kurithi nafasi ya Sata, ikizingatiwa kuwa Dkt. Scott asingeweza kugombea kwa sababu wazazi wake hawakuzaliwa Zambia.

Nini kinafuata katika simulizi hii ya kusisimua juu ya maisha, mikasa na utata wa kifo na maziko ya Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu? Usikose.

Related articles

Recent articles