32.7 C
New York

Mradi wa maziwa waiongezea tija Tanzania

Published:

Na Mwandishi Wetu, Tanga

SERIKALI imeomba kuendelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ireland kupitia Awamu ya Pili ya Mradi wa Maziwa Faida kuanzia mwaka 2027 hadi 2032, kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuboresha kipato cha wafugaji na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya mifugo.

Ombi hilo limetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Fabian Madele, wakati akifungua Maonesho ya Ubunifu na Teknolojia katika Sekta ya Maziwa (TALIRI Open Day 2026) yaliyofanyika katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki, jijini Tanga.

Dkt. Madele amesema ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania kupitia TALIRI na Taasisi ya Maendeleo ya Kilimo na Chakula ya Ireland (TEAGASC), unaofadhiliwa na Serikali ya Ireland, umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya maziwa hususan katika Mkoa wa Tanga na maeneo mengine yaliyofikiwa na mradi huo.

Amesema kabla ya kuanza kwa mradi huo, wafugaji wengi walikuwa wakipata wastani wa lita tatu hadi tano za maziwa kwa ng’ombe mmoja kwa siku, lakini kupitia matumizi ya malisho bora, teknolojia za kisasa za ufugaji, huduma za ugani na mafunzo kwa wafugaji, uzalishaji umeongezeka hadi kufikia wastani wa lita 15 kwa ng’ombe mmoja kwa siku.

“Matokeo haya yanaonesha wazi mchango mkubwa wa utafiti, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa katika kuongeza tija, kuboresha kipato cha wafugaji na kuimarisha usalama wa chakula na lishe nchini,” amesema Dk. Madele.

Amesema mafanikio hayo yanakuja wakati Tanzania ikiwa bado na pengo kubwa la uzalishaji wa maziwa, ambapo kwa sasa nchi inazalisha takribani lita bilioni 4.1 kwa mwaka dhidi ya mahitaji ya zaidi ya lita bilioni 13, hali inayodhihirisha fursa kubwa ya uwekezaji katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Suzanne Keatinge, ameipongeza TALIRI kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kueleza kuwa mafanikio yaliyopatikana yanaonesha umuhimu wa uwekezaji katika tafiti na teknolojia za kisasa za kilimo na mifugo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Profesa Erick Komba, amesema mafanikio ya Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Maziwa Faida uliotekelezwa kati ya mwaka 2021/2022 na 2025/2026 yameweka msingi imara wa kuendelea kuleta mapinduzi katika sekta ya maziwa nchini.

Amesema mradi huo uliogharimu zaidi ya Euro milioni tatu, sawa na zaidi ya Sh bilioni saba, umewanufaisha zaidi ya wanawake na vijana 3,000 katika ukanda wa pwani ya mashariki, hususan Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa Profesa Komba, mradi huo umewezesha kufanyika kwa tafiti za malisho yanayostahimili mazingira ya ukanda wa pwani, kubainisha aina bora za ng’ombe wa maziwa, kuwajengea uwezo maafisa ugani, kuimarisha vyama vya ushirika vya wafugaji na kuanzisha mashamba darasa yanayotumika kusambaza teknolojia za kisasa za ufugaji.

Amesema TALIRI itaendelea kuhakikisha matokeo ya tafiti na ubunifu unaozalishwa yanawafikia wafugaji wengi zaidi ili kuongeza uzalishaji, tija na ushindani wa sekta ya maziwa nchini.

Mradi wa Maziwa Faida umetajwa kuwa moja ya mifano bora ya ushirikiano wa maendeleo unaotumia utafiti, ubunifu na teknolojia kutatua changamoto za uzalishaji wa maziwa na kuimarisha mchango wa sekta ya mifugo katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Related articles

Recent articles