MOGADISHU, Somalia
GUMZO kubwa kuelekea fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu ni mwamuzi wa kati raia wa Somalia, Omar Artan, kurejea nchini kwao baada ya kunyimwa kibali cha kuingia Marekani, hivyo kuikosa michuano hiyo.
Artan alikuwa sehemu ya waamuzi saba wa Afrika walioteuliwa kuchezesha michuano hiyo, wengine wakiwa wanatoka katika mataifa ya Algeria, Misri, Gabon, Mauritania, Morocco na Afrika Kusini.
Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 34, alizuiwa mpakani katika Uwanja wa Ndege mjini Miami, licha ya kuwa na hati ya kusafiria ya kidiplomasia.
Ifahamike kuwa waamuzi wote wako Miami kwa ajili ya mafunzo na maandalizi ya fainali hizo zitakazoanza Juni 11, 2026, zikifanyika Marekani, Mexico na Canada.
“FIFA inathibitisha kuwa mwamuzi Omar Abdulkadir Artan hatoweza kufanya mazoezi na kuchezesha mechi za Kombe la Dunia baada ya kunyimwa kibali cha kuingia Marekani,” ilieleza taarifa ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
NDOTO ILIYOOTA MBAWA
Refa huyo aliyepata beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwaka 2018 alitarajiwa kuwa refa wa kwanza raia wa Somalia kuchezesha mashindano ya Kombe la Dunia.
Ikumbukwe, Artan ndiye mwamuzi bora Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa mwaka 2025 na alichezesha mechi mbili wakati wa fainali za AFCON zilizopita.
Januari, 2024, aliandika historia ya kuwa mwamuzi wa kati wa kwanza raia wa Somalia kuchezesha michuano ya AFCON alipopewa mchezo wa Kundi E uliozikutanisha Tunisia na Namibia.
Ikumbukwe pia, Mei, 2026, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilimkabidhi fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya AS FAR ya Morocco na vigogo wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns.
Kabla ya Kiongozi wa Waamuzi wa FIFA, Pierluigi Collina, kumteua kwenda Kombe la Dunia, Artan alikuwa sehemu ya waamuzi waliochezesha fainali hizo kwa vijana wa U-20 mwaka 2025.
Ni baada ya kuteuliwa kwa ajili ya Kombe la Dunia, ndipo Rais wa Somalia, Hassan Mohamud, alipomtaja kama mfano wa kuigwa kwa kizazi kipya cha Somalia.
KWANINI MAREKANI IMEMZUIA?
Ni suala la kisiasa. Somalia iko kwenye orodha ya nchi zilizowekewa kizuizi cha raia wake kuingia Marekani chini ya utawala wa Rais wa sasa, Donald Trump.
Artan, katika mahojiano yake na Gazeti la New York Times, amesema alihojiwa kwa saa 11 na maofisa wa mpakani mjini Miami.
Kwa mujibu wake, maswali mengi aliyoulizwa mpakani yalihusiana na Kundi la kigaidi la Al-Shabab linalotajwa kuwa na uhusiano wa karibu na Al-Qaeda.
Kabla ya kukutana na kisanga hicho, Artan alikuwa na furaha na shahuku kubwa ya kuwa sehemu ya waamuzi wa mashindano hayo makubwa.
“Ndoto ya kila mwamuzi ni kuchezesha Kombe la Dunia. Unapoteuliwa, unapata hisia kuwa jitihada ulizofanya zimelipa,” alisema katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Kabla ya kukumbana na kile kilichotokea, Artan alikuwa Uturuki kwa maandalizi ya Kombe la Dunia. “Maandalizi ya Kombe la Dunia siyo kazi ndogo; kimwili, kiakili na kiweledi,” alisema.
“Katika Kombe la Dunia, unakutana na waamuzi wa daraja la juu. Unatakiwa uwe na viwango hivyo,” alisema Artan akiwa Uturuki wakati huo.
KWANINI FIFA HAIWEZI KUMNASUA?
Katika taarifa yake baada ya Artan kuzuiwa, FIFA ilisema: “FIFA haihusiki katika michakato ya uhamiaji ya nchi husika, ikiwamo utoaji wa viza … Mwenyeji ndiye anayeamua nani wa kumpa viza na nani wa kuingia nchini kwake.”
Kwa upande wake, Serikali ya Somalia imeeleza kusikitishwa kwake na kitendo hicho, wakati huo Artan akisema anaishukuru familia ya soka duniani kote kwa kumtumia meseji za kumfariji.
“Ningependa kuwashukuru FIFA na CAF kwa sapoti na naahidi kuendeleza kiwango changu kizuri cha uchezeshaji katika mechi zijazo. Nawatakia kila la kheri wenzangu watakaokwenda Kombe la Dunia, tukutane katika michuano ijayo,” amesema Artan.
Wakati huo huo, chanzo cha ndani kutoka Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kimeeleza kuwa Taasisi hiyo imesikitishwa na hatua ya Marekani kumzuia Artan lakini haina mamlaka ya kupingana na uamuzi huo.
MAJERAHA YALIMSTAAFISHA KUCHEZA
Aliamua kujitosa katika taaluma ya uamuzi baada ya majeraha ya mguu kumzuia kuendelea na maisha yake ya kucheza soka.
Akivutiwa na aliyekuwa kiongozi wa waamuzi nchini Somalia wakati huo, Osman Jama Dirac, alianzia katika mechi za mtaani mjini Mogadishu, kabla ya kuaminika na kupewa mashindano makubwa.
“Alikuwa ni kama baba kwetu (waamuzi). Hakuwa kiongozi wa waamuzi tu, bali alitujali. Kama ulikuwa Mogadishu na hauna kitu, angehakikisha unakula kwa kukupeleka mgahawani,” alisema.
Hata hivyo, Dirac aliuawa Agosti, 2017, na hiyo ikawa habari mbaya kwa Artan. “Ilikuwa ngumu sana (kupokea taarifa hiyo). Alikuwa ananiandaa kuwa mwamuzi wa kimataifa. Angefurahi sana kuona Somalia imefika hapa ilipo,” alisema.


