Na Mwandishi Wetu,Gazetini
WAKATI maelfu ya vijana wa Kitanzania wakiendelea kuingia katika soko la ajira kila mwaka huku nafasi rasmi za ajira zikibaki finyu, wataalamu wa masuala ya kazi na ajira wameonya kuwa uhamiaji wa wafanyakazi umeendelea kuwa sehemu muhimu ya uchumi na maisha ya jamii inayohitaji usimamizi madhubuti, sera bora na utoaji sahihi wa taarifa kwa umma.
Masuala hayo yamejadiliwa leo Juni 10, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao kifupi kilichowakutanisha wanahabari, Serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi kujadili utawala wa uhamiaji wa kazi Tanzania na Ukanda wa Pembe ya Afrika Mashariki (EAHoA), kilichoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Akizungumza katika kikao hicho, Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa ILO, Aida Awel, amesema uhamiaji wa kazi ni moja ya masuala makubwa duniani na katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na ongezeko la watu wanaovuka mipaka kutafuta ajira, elimu, usalama na maisha bora.
Amesema kila mwaka mamilioni ya watu katika ukanda huo huhama kwa sababu mbalimbali za kiuchumi na kijamii, huku nyuma ya takwimu hizo kukiwa na simulizi za maisha ya watu halisi.
“Nyuma ya kila takwimu ya uhamiaji kuna simulizi ya kibinadamu. Hawa ni vijana wanaotafuta ajira zao za kwanza, wazazi wanaotafuta namna ya kuhudumia familia zao na wafanyakazi wanaopigania utu na maisha bora,” amesema Awel.
Amesema Tanzania imekuwa katika nafasi muhimu ndani ya mfumo wa uhamiaji wa kikazi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya vijana wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka huku wengi wakikumbana na changamoto za ukosefu wa ajira rasmi, kutokuwapo kwa taarifa sahihi za soko la ajira na kutolingana kwa ujuzi na mahitaji ya kazi.
Kutokana na hali hiyo, amesema uhamiaji wa kazi umegeuka kuwa mkakati muhimu wa kujikimu kwa familia nyingi za Kitanzania.
“Tanzania inaendelea kushuhudia wananchi wake wakitafuta fursa za kazi ndani ya Afrika Mashariki na hata katika nchi za Ghuba. Wakati huo huo, nchi inapokea pia wafanyakazi kutoka mataifa jirani wanaochangia katika sekta za kilimo, ujenzi, biashara, usafirishaji, utalii na kazi za majumbani,” alisema.
Awel amewataka wanahabari kuandika habari za uhamiaji kwa usahihi na uwajibikaji ili kupunguza upotoshaji wa taarifa, kuvunja dhana potofu dhidi ya wahamiaji na kusaidia kujenga mshikamano wa kijamii.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Oddo Hekela, amesema Tanzania haiendeshi uchumi wake kwa kutegemea fedha zinazotumwa na wahamiaji wanaofanya kazi nje ya nchi kama ilivyo kwa baadhi ya mataifa mengine.
“Kipaumbele chetu kikuu ni ulinzi wa wafanyakazi. Ingawa uhamiaji unachangia maendeleo ya uchumi, Tanzania inaendelea kuweka mkazo katika kulinda haki, utu na ustawi wa wafanyakazi,” amesema Hekela.
Amesema Tanzania ni nchi inayotuma na kupokea wafanyakazi, hivyo tayari imeweka mifumo ya kisheria inayosimamia ajira za wageni, huduma za ajira, mahusiano kazini pamoja na sheria za kupambana na biashara haramu ya binadamu.
Hata hivyo, amewataka wanahabari kuwa makini katika matumizi ya lugha wanaporipoti habari za uhamiaji kwa kuepuka kutumia neno “mhamiaji haramu”.
“Lugha tunayotumia ina umuhimu mkubwa. Tunapaswa kuzungumzia hadhi ya uhamiaji badala ya kuwapa watu majina yanayoweza kuwanyima utu wao,” amesema.
Hekela pia amewataka waandishi wa habari kwenda zaidi ya kuripoti matukio na kuanza kufanya uchambuzi wa kina kuhusu sera, sheria na mifumo inayounda mazingira ya uhamiaji wa kazi nchini.
“Uandishi wa habari si kuripoti matukio pekee. Ni pamoja na kufanya uchunguzi, tafsiri na kusaidia umma kuelewa sheria na mifumo iliyopo nyuma ya matukio hayo,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya wafanyakazi, Mkurugenzi wa Jinsia, Wanawake na Vijana wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nasra Shargy, amesema ukuaji wa uhamiaji wa kazi umeleta fursa za kiuchumi lakini pia umeongeza hatari za unyonyaji, biashara haramu ya binadamu na ukiukwaji wa haki za wafanyakazi.
“Kama vyama vya wafanyakazi tunaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ulinzi wa wafanyakazi wahamiaji. Uhamiaji salama unahitaji ushirikiano wa wadau wote,” alisema.
Amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kutoa elimu kwa umma kuhusu ajira za nje, kufichua udanganyifu wa mawakala wasio waaminifu na kuwasaidia wafanyakazi kuelewa haki zao kabla ya kuamua kuhama kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
“Uandishi wenye uwajibikaji unaweza kuwasaidia wafanyakazi kufanya maamuzi salama, kuelewa haki zao na kuzitaka taasisi husika kuwajibika,” amesema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Utetezi wa Sera wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Renatus Mbamilo, amesema uhamiaji wa kazi ni suala lenye sura nyingi linalohitaji uchambuzi wa kina na taarifa zinazotegemea ushahidi.
Amesisitiza kuwa wanahabari wanapaswa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa ikiwemo Serikali, waajiri, mawakala wa ajira, wahamiaji waliorejea nchini na taasisi za maendeleo ili kuandika habari zenye uwiano na zinazosaidia jamii kuelewa hali halisi ya uhamiaji wa kazi.
“Uhamiaji si suala la Watanzania kwenda kufanya kazi nje pekee, bali pia linahusu wafanyakazi wa kigeni wanaochangia uchumi wa Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ujenzi, biashara, utalii na huduma,” amesema.
Mkutano huo ulihitimishwa kwa wadau kutaka kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, waajiri, vyama vya wafanyakazi, taasisi za maendeleo na vyombo vya habari ili kujenga mfumo salama, wenye haki na unaozingatia utu katika usimamizi wa uhamiaji wa kazi nchini.


