17.4 C
New York

Wanawake watajwa chachu ya mafanikio katika operesheni za kulinda amani duniani

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WANAWAKE wameelezwa kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha amani, usalama na ustawi wa jamii, huku ushiriki wao katika operesheni za kulinda amani ukitajwa kuwa kichocheo cha mafanikio katika kuzuia migogoro, kujenga amani na kurejesha utulivu katika maeneo yenye machafuko.

Hayo yamesemwa juzi jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Afisa Mwanafunzi (TMA) cha Kijeshi, Meja Jenerali Jackson Mwaseba wakati akifunga kozi ya pili ya wanawake katika masuala ya amani na Usalama (Women, Peace and Security – WPS).

Kozi hiyo imefanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC) kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN Women).

Jumla ya washiriki 27 kutoka vyombo vya ulinzi na usalama nchini ambavyo ni maofisa na askari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Magereza waliweza kupata fursa ya kushiriki katika mafunzo hayo yaliyoanza Mei 27, 2026 hadi Juni 5,2026.

Akizungumza mara baada ya kufunga kozi hiyo, Meja Jenerali Mwaseba amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi na usalama ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa ajenda ya wanawake, amani na usalama inatambua nafasi ya kipekee ya wanawake katika kuzuia migogoro, kushiriki katika operesheni za kulinda amani, kutatua migogoro na kusaidia jamii kupona baada ya migogoro.

Meja Jenerali Mwaseba amebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, ambalo linahimiza ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani na maamuzi ya kiusalama.

Amesema juhudi za kimataifa zimeongeza ushiriki wa wanawake katika misheni za kulinda amani na kusaidia kuingiza mtazamo wa kijinsia katika utekelezaji wa majukumu hayo.

“Wanawake wana nafasi ya kipekee katika kujenga imani na mawasiliano na jamii wanazozihudumia, hasa wanawake na watoto ambao mara nyingi huathirika zaidi na migogoro. Wanajisikia huru zaidi kushirikiana na maafisa wanawake kwa sababu wanaelewa changamoto zao kwa karibu zaidi,” amesema

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwawezesha wanawake kushiriki kwa kiwango kikubwa zaidi katika operesheni za kulinda amani kupitia ajira, mafunzo, ushauri wa kitaalamu na sera zinazozingatia usawa wa kijinsia.

Aidha, amesema matokeo ya mafunzo hayo yataongeza idadi ya wataalamu wa masuala ya jinsia na walinda amani wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi katika misheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa.

“Mafanikio ya kozi hii ni ushahidi wa dhamira ya washirika wetu katika kuimarisha uwezo wa taifa letu na kuendeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama nchini Tanzania,” amesema.

Hata hivyo aliwapongeza washiriki wote waliomaliza mafunzo hayo, akisema mafanikio yao ni matokeo ya nidhamu, kujituma, uvumilivu na ari ya kufikia ubora katika kazi zao.

Alieleza kuwa maarifa na ujuzi walioupata katika kipindi cha wiki mbili za mafunzo utasaidia kuimarisha juhudi za kulinda amani na usalama katika taasisi zao na maeneo wanayohudumia, pamoja na kuwawezesha kutoa elimu hiyo kwa wenzao kabla ya kushiriki katika misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Naye Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema kuwa ushiriki wa wanawake katika masuala ya amani na usalama ni nguzo muhimu katika kuimarisha ufanisi, uhalali na uendelevu wa operesheni za kulinda amani na michakato ya maamuzi.

Brigedia Jenerali Itag’are amesema mafanikio ya kozi hiyo yametokana na maono, kujitolea na ushirikiano wa wadau mbalimbali waliochangia kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

Aidha, ametoa pongezi kwa UNDP na Serikali ya Japan kwa kuendelea kuunga mkono shughuli za TPTC, akisema mafanikio ya kozi hiyo ni ushahidi wa dhamira yao ya kuona kituo hicho kinaendelea kukua na kuwa kitovu muhimu cha mafunzo ya kulinda amani.

Aliwapongeza washiriki wote wa mafunzo hayo kwa ushiriki wao mkubwa na mijadala yenye tija iliyochangia kubadilishana uzoefu na maarifa. Alieleza kuwa tofauti na kozi ya kwanza iliyowahusisha maafisa wanawake kutoka JWTZ pekee, safari hii washiriki walitoka katika taasisi mbalimbali.

Kwa mara ya kwanza pia, kozi hiyo iliwashirikisha wanaume wachache, hatua aliyosema inaonesha umuhimu wa ushirikishwaji wa kila kundi katika kutekeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama.

Related articles

Recent articles