LONDON, Uingereza
MIAKA ya hivi karibuni imewashuhudia makocha waliokabidhiwa mikoba ya kuzinoa timu kubwa za Ligi Kuu ya England (EPL) wakipitia nyakati ngumu, wengi wakishindwa kumaliza misimu miwili katika benchi.
David Moyes aliajiriwa Manchester United mwaka 2013 akichukua nafasi ya Alex Ferguson aliyestaafu. Alipewa mkataba wa miaka sita lakini alifanya kazi miezi 10 tu.
Moyes, ambaye ni raia wa Scotland kama alivyo Ferguson, alifukuzwa baada ya timu hiyo kukosa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1995.
Kwa hivi karibuni, Ruben Amorim alitimuliwa akiwa ameinoa Man United kwa miezi 18 tu, kisha Michael Carrick kupewa kibarua cha muda, kabla ya kusainishwa miaka miwili kwa ajili ya msimu ujao (2026-27).
Roy Hodgson, kwa upande wake, Liverpool walimpa ajira Julai, 2010 baada ya kocha huyo raia wa England kuiongoza Fulham kufika fainali ya Ligi ya Europa. Alifukuzwa mwaka mmoja tu baadaye.
Hivi karibuni, majanga ya aina hiyo yalimkuta Arne Slot, kocha raia wa Uholanzi, ambaye amedumu Anfield kwa misimu miwili tu.
Graham Potter, ambaye Chelsea walimtoa Brighton, alibeba matarajio makubwa lakini kocha huyo alifungashiwa virago akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi 22 tu za EPL.
Majanga yaliwakuta pia Enzo Maresca aliyedumu msimu mmoja na Frank Lampard aliyetimuliwa baada ya miezi 18 tu ya kufanya kazi Stamford Bridge.
Tottenham nayo imeshuhudia makocha wakiingia na kutimuliwa ndani ya muda mfupi, kama ilivyowatokea Nuno Santo raia wa Ureno na Thomas Frank wa Denmark.
Je, Andoni Iraola anayetarajiwa kuanza kazi Liverpool ataweza kuepuka kile kilichowakuta wenzake hao? Kocha huyo aliyeondoka Bournemouth anakwenda kuziba pengo la Slot.


