Na mwandishi wetu, Gazetini
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema hakuna taifa linaloweza kubaki nyuma katika dunia ya sasa inayotawaliwa na teknolojia, akili bandia (AI), sayansi ya data, roboti na ubunifu wa kisasa.
Akizungumza Juni 4, 2026 katika Chuo Kikuu cha RUDN nchini Urusi, katika mwendelezo wa ziara yake ya kitaifa ya siku tano, Samia alisema Tanzania na Afrika kwa ujumla zinapaswa kuwaandaa vijana kuongoza katika uchumi wa maarifa badala ya kuwa watazamaji wa mabadiliko ya dunia.
“Hakuna taifa duniani linaloweza kumudu kubaki nyuma. Swali kwa Tanzania na Afrika si kama tutashiriki katika uchumi wa maarifa, bali ni namna tutakavyowaandaa vijana wetu kuongoza katika dunia inayobadilika,” alisema Samia.
Rais huyo alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu kuwa msingi wa mageuzi ya taifa, huku akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupimwa kwa uwepo wa miundombinu pekee.
“Miundombinu peke yake haiwezi kubadilisha taifa. Tunahitaji watu wenye ujuzi, nidhamu, ubunifu na uzalendo wanaoelewa kuwa maarifa yanapaswa kutumikia manufaa ya jamii,” alisema.
Katika hotuba yake, Samia aliutaja Mpango wa Samia Scholarship ulioanzishwa mwaka 2023 kuwa sehemu ya uwekezaji wa taifa kwa vijana wenye vipaji, hasa wanaotoka familia zenye uwezo mdogo.
Alisema zaidi ya wanafunzi 5,000 tayari wamefaidika na mpango huo katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi na tiba.
“Tunafanya uwekezaji kwa daktari atakayeokoa maisha, mhandisi atakayejenga miundombinu, mwanasayansi atakayesuluhisha changamoto na mbunifu atakayezalisha ajira,” alisema.
Samia pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa elimu kati ya Tanzania na Urusi kupitia tafiti za pamoja, kubadilishana wanafunzi na wahadhiri pamoja na kuongeza nafasi za ufadhili wa masomo.


