Na Hassan Mwasha,Gazetini
KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa, amesema kuimarika kwa Chama hicho chini ya Mwenyekiti Tundu Lisu ndiyo sababu ya kurudi kwake kundini.
Aidha, Mchungaji Msigwa ameeleza kuwa aliondoka CHADEMA baada ya kuona kimepoteza mwelekeo, tofauti na madai ya wengi kwamba alikwenda CCM kwa tamaa ya fedha na nafasi ya uongozi.
Mchungaji Msigwa ameyasema hayo leo Juni 2, 2026 katika mahojiano yake na kituo cha redio cha Wasafi FM.
Alitua CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, hatua iliyokuja baada ya kulalamikia ‘figisu’ katika Uchaguzi wa Kanda ya Nyasa ndani ya CHADEMA, ambapo alibwagwa na Joseph Mbilinyi.
Akizungumzia kuondoka kwake, Mchungaji Msigwa amesema ni uamuzi ulitokana na kutokuridhishwa na mwenendo wa CHADEMA wakati huo.
“Niliondoka CHADEMA baada ya kuona Chama ‘kime-compromise’ (kimeingia makubaliano na CCM). Ukiitazama CHADEMA ya sasa, ni tofauti na ile iliyokuwa ikienda kiujanjaujanja,” amesema.
Aidha, Mchungaji Msigwa amesema amekuwa mbunge kwa miaka mingi na hata Waziri kivuli Bungeni, hivyo hakwenda CCM kufuata fedha au cheo cha kisiasa.
“Nimekuwa mbunge, nimekuwa Waziri kivuli. Siendeshwi na tamaa ya cheo. Maisha yangu, thamani yangu haviendeshwi na vyeo. Kama ni fedha, ningebaki CCM. Huku CHADEMA hakuna vyeo wala fedha.
“Dhamira ndiyo iliyonisukuma kurudi CHADEMA. Siwezi kukubali kuwa sehemu nisiyo na amani ili kufurahisha watu. Ndiyo maana nimeomba radhi,” amesema.
Katika hatua nyingine ya mahojiano yake na Wasafi FM, Mchungaji Msigwa amekiri kujutia uamuzi wa kwenda CCM, akisema anatamani angejipa muda wa kutafakari kabla ya kuchukua uamuzi huo.
Amesema: “Nafikiri nilitaka kujiponya baada ya maumivu niliyokuwa nayo wakati huo. Lakini, wakati ule akiwa kocha wa Manchester United, Alex Ferguson alisema hakuna mtu mkubwa kuliko klabu.
“Nadhani ningefanya maamuzi tofauti kuliko kuondoka CHADEMA na kwenda CCM. Ndiyo maana nimeomba radhi.”
Kwa upande mwingine, Mchungaji Msigwa aliulizwa kilichomsukuma kurudi CHADEMA, badala ya kuibukia chama kingine cha upinzani baada ya kuondoka CCM.
“Kwa mtazamo wangu, Chama pekee cha upinzani ni CHADEMA. Nimekuwa kwenye siasa kwa miaka mingi, navijua vyama vya mifukoni. Siwezi kuungana navyo. Ukitaka kuona ukubwa wa CHADEMA, angalia kinavyoandamwa,” amesema.
Pia, Mchungaji Msigwa aligusia maisha yake mapya ndani ya CHADEMA, ikiwamo uhusiano na viongozi, akiwamo Joseph Mbilinyi aliyembwaga katika Uchaguzi wa Kanda ya Nyasa mwaka 2025.
“Kwa wanachama, lazima nikiri kuwa yapo makundi: wapo walioniamini na kunipokea vizuri kwa kunitumia jumbe za kunipa moyo.
“Pia, wapo walioniponda, na wapo wenye shaka. Makundi yote hayo ya haki katika kile yanachokiamini. Naomba wanipe muda, watajua kama nadanganya au la,” amesema.
Akizungumzia uhusiano wake na viongozi, akiwamo Mbilinyi ‘Sugu’, Mchungaji Msigwa amesema: “Tulipishana wakati ule. Tumemaliza na tuko kwenye uhusiano mzuri.”


