MAPUTO, Msumbiji
KWA siku za hivi karibuni, yamezuka matukio ya wanasiasa wa upinzani nchini Msumbiji kuuawa kwa kupigwa risasi.
Mei 9, 2026, Anselmo Vicente, ambaye ni mratibu wa Chama cha National Alliance for a Free and Autonomous Mozambique (ANAMOLA), aliuawa kwa kupigwa risasi katika Jimbo la Manica katikati mwa Msumbiji.
Polisi walithibitisha kutokea kwa tukio hilo, taarifa yake ikieleza kuwa mwanasiasa huyo aliuawa wakati akirejea nyumbani kwake akitokea kwenye kikao cha Chama.
Wiki moja baadaye, Mei 15, mwanachama mwengine wa ANAMOLA, Pedro Chauke, aliuawa kwa staili hiyo ya kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake katika Jimbo la Gaza.
Matukio hayo ni mfululizo wa wanachama wa ANAMOLA kuandamwa tangu Chama hicho kilipoanzishwa na mwanasiasa Venancio Mondlane mwaka 2025.
ANAMOLA hakina mbunge kwa sasa, wakati huo Chama tawala, FRELIMO, ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1975, kina wawakilishi 171 kati ya 250 waliopo.
Wengine wanatoka vyama vitatu vya Optimist Party for the Development of Mozambique (PODEMOS), RENAMO na Democratic Movement of Mozambique (MDM).
Kwa mujibu wa Mondlane, mwaka mmoja wa uhai wa Chama chake cha FRELIMO kimeshuhudia kuuawa kwa wanachama wake 56 na wengine 436 wakipitia madhila mbalimbali, ikiwamo kutekwa.
“Serikali inahusika katika haya mauaji. Tumewawilisha ushahidi wote lakini hakuna hatua zilizochukuliwa,” amesema.
Kwa upande wake, Judite Macuacua wa MDM amedai kuwa kuikosa Serikali iliyoko madarakani ni kosa linaloweza kusababisha hukumu ya kifo nchini Msumbiji.
Wakati siasa za upinzani zikipitia kadhia hiyo, hali ya uhuru wa kujieleza nayo imekosolewa mara kadhaa na wanaharakati wa haki za binadamu wa nje na ndani ya Msumbiji.
Tangu mwaka 2015, wanaharakati na waandishi wa habari wamekuwa wakifuatiwa kwa karibu na vyombo vya dola vinavyotajwa kukilinda zaidi Chama tawala, FRELIMO.
“Nchini Msumbiji, kuna ukandamizwaji mkubwa wa kisiasa. Hii ilikuwepo tangu wakati wa mfumo wa Chama kimoja na haijabadilika hata baada ya ujio wa vyama vingi,” anasema Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia mjini Maputo, Adriano Nuvunga.
Anaongeza: “Kuna mauaji yanayofanyika hapa Msumbiji. Vikundi vya mauaji vinaratibiwa na Serikali. Wanaua ili kuwatia hofu, kuharibu upinzani na kuwazuia watu kujihusisha na siasa.”
Hata hivyo, kama ambavyo imefanya mara zote, Serikali imekanusha kujihusisha na vitendo vya mauaji ya wakosoaji wake, licha ya kutokuwapo kwa matokeo ya kuridhisha katika kile inachokiita uchunguzi wa kubaini wahusika.


