Na Malima Lubasha, Serengeti
WAUMINI wa dini ya Kiislamu wilayani Serengeti mkoani Mara wametakiwa kuendeleza ibada, kudumisha umoja, upendo na mshikamano ili kuendelea kulinda amani na kuchochea maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa juzi na Sheikh wa Wilaya ya Serengeti, Sheikh Juma Simba, wakati wa Baraza la Idd lililofanyika katika Msikiti wa Masjid Noor mjini Mugumu baada ya kukamilika kwa ibada ya Hijja.
Akizungumza katika baraza hilo, Sheikh Simba amesema Waislamu wanapaswa kuadhimisha sikukuu hiyo kwa upendo, ushirikiano na kufanya matendo mema kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Amesema ni muhimu kwa waumini kuendelea kuwa na moyo wa kusaidiana, kuheshimiana na kushikamana ili kuimarisha maendeleo ya dini pamoja na jamii.
“Bila kuwepo kwa umoja, upendo na ushirikiano miongoni mwa waumini, maendeleo ya kiuchumi na miradi ya uzalishaji mali hayawezi kufanikiwa. Ili tufikie maendeleo tunayoyataka lazima tuendelee kudumisha mshikamano na kulinda amani ya taifa,” amesema Sheikh Simba.
Aidha, amewahimiza waumini kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Kiislamu ikiwemo miradi ya elimu, ujenzi wa misikiti na vibanda vya biashara inayolenga kukuza uchumi wa jamii ya Kiislamu.
“Maendeleo haya tunayoyaona, ikiwemo ujenzi wa madarasa, vyoo, misikiti na vibanda vya biashara, yametokana na mchango wa waumini wenyewe. Nawapongeza wote kwa kujitoa kwenu,” amesema.
Kwa upande wake, mmoja wa waumini, Ustadh Hashimu Remmy, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanapata elimu ya dini pamoja na elimu ya kawaida ili kujenga jamii yenye maadili mema.


