AMSTERDAM, Uholanzi
KWA Taifa kama Uholanzi, ambalo historia yake ya kuzalisha vipaji vikubwa vya soka inafahamika, inaweza kushangaza kuona haijwahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.
Licha ya kushiriki mara 11 (1934, 1938, 1974, 1978, 1990, 1994, 1998, 2006, 2010, 2014 na 2022) imefika fainali mara tatu pekee (1974, 1978, 2010).
Kwa wachambuzi wa soka barani Ulaya, wanaitaja ‘Orange’ kuwa ni timu ya Taifa bora kutokuwahi kuchukua ubingwa wa fainali hizo.
Si tu Kombe la Dunia, Uholanzi, Taifa lenye watu milioni 18.4, limekuwa halina mafanikio hata kwenye fainali za EURO. Ni mabingwa mara moja pekee (1988) katika historia ya michuano hiyo.
Baada ya kukosa tiketi mwaka 2018 nchini Urusi, Uholanzi walirejea Kombe la Dunia mwaka 2022 kule Qatar na safari yao kuishia hatua ya robo fainali.
Safari hii, walilazimika kusubiri hadi mechi ya mwisho (dhidi ya Lithuania) kujihakikishia tiketi ya kucheza Kombe la Dunia. Walishinda mabao 4-0 na kukaa kileleni mwa Kundi G, wakikusanya pointi 20 dhidi ya 17 za Poland iliyoshika nafasi ya pili.
Wataivaa Japan katika mechi yao ya kwanza itakayochezwa Juni 14, kabla ya kuzikabili Sweden (Juni 20) na Tunisia (Juni 25).
Virgil van Dijk, beki kisiki wa Liverpool na mshindi wa mataji ya Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu ya England, anatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwao kwenye eneo la ulinzi. Ana uzoefu wa mechi 88 akiwa na kikosi cha Uholanzi.
Eneo la kiungo linamtegemea staa wa Barcelona, Frenkie de Jong, ambaye amekuwa mchezaji muhimu kwa Uholanzi tangu alipoanza kuitumikia mwaka 2018.
Aidha, kiongozi wa safu ya ushambuliaji ni Memphis Depay. Uzoefu wake wa kuzitumikia PSV, Manchester United, Lyon, Barcelona na Atletico Madrid una maana kubwa kwa Uholanzi. Ana mabao 55 akiwa na kikosi hicho.
Wakati huo huo, wanaye kocha mzoefu kwenye benchi la ufundi, Ronald Koeman, ambaye aliinoa aliondoka mwaka 2020 na kurejea mwaka 2023.
Baada ya miaka mingi ya kupotea, aliirejesha Uholanzi katika michuano ya kimataifa, ilipofuzu fainali za EURO za mwaka 2020.
Koeman, ambaye alikuwa mchezaji wakati Uholanzi ilipotwaa ubingwa wa EURO mwaka 1988, ni kocha aliyewahi kupita Everton, Southampton na Barcelona aliyoipa taji la Copa del Rey mwaka 2021.


