LONDON, Uingereza
UKARIBU wa wachezaji wa soka na makocha wao hauishii uwanjani tu, bali wakati mwingine huenda mbali zaidi na kufika hadi ngazi ya familia.
Lakini, ukaribu huo umezalisha mara kadhaa mahusiano ya kimapenzi kati ya wanasoka na watoto wa kike wa makocha wao. Endelea kusoma.
RONALDINHO ‘GAUCHO’
Ndicho kilichotokea kwa kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Ronaldinho, akiwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Barcelona kuanzia mwaka 2003 hadi 2008.
Wakati huo kocha akiwa Frank Rijkaard, Ronaldinho ‘alijiongeza’ na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na binti wa Mholanzi huyo. Bibiye anaitwa Lindsay Rijkaard.
Hata hivyo, uhusiano na binti yake haukumfanya Rijkaard amchukie ‘Gaucho’ na badala yake aliendelea kuwa naye karibu, ikiwamo kumtumia katika kikosi cha kwanza.
Nyota huyo aliwahi kumzungumzia Rijkaard akisema: “Kilikuwa ni kipindi kizuri (kufanya kazi na kocha huyo). Alikuwa kocha bora zaidi kuwahi kuwa naye kwenye timu.”
SERGIO ‘KUN’ AGUERO
Mwaka 2008, wakati Aguero akiwa chini ya Diego Maradona aliyekuwa akiinoa timu ya Taifa ya Argentina, alianzisha uhusiano na binti wa kocha huyo aitwaye Gianinna.
Walibahatika kupata mtoto mmoja wa kiume, Benjamin, kabla ya wawili hao kuachana mwaka 2012, chanzo kikitajwa kuwa ni tabia za usaliti za Aguero.
Baada ya kuachana na binti yake, Maradona (sasa marehemu) aliendelea kumchukia Aguero na wakati fulani alisema anajuta kumfahamu mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester City.
FERRAN TORRES
Wakati wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 nchini Qatar, zilivuma taarifa za mshambuliaji huyo kuwa kwenye uhusiano na binti wa Luis Enrique aitwaye Sira Martinez.
Ni wakati huo, Enrique alikuwa kocha wa Torres katika kikosi cha timu ya Taifa ya Hispania. Kwa mujibu wa ripoti, ukaribu wake na mrembo huyo ulianza mwaka 2021.
NICKLAS BENDTNER
Mshambuliaji wa kati wa zamani wa Washika Bunduki wa Kaskazini mwa Jiji la London, Arsenal, na timu ya Taifa ya Denmark.
Bendtner akiwa kwa mkopo Birmingham City, ‘alijilipua’ kwa kuanzisha ukaribu wa kimapenzi na binti wa aliyekuwa kocha wa timu hiyo wakati huo, Steve Bruce.
Ilianza kama utani, kabla ya Bendtner kujikuta ‘amezama’ kwenye penzi la mrembo huyo, ingawa ripoti zinaeleza kuwa walikuja kuachana mwaka 2008.


