12.9 C
New York

Vilio, simanzi vyatawala msibani kwa mmiliki wa kiwanda cha XIL LI

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

VILIO na simanzi vilitawala katika eneo la kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL LI kilichopo Mabibo Sokoni, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, baada ya ndugu, wafanyakazi na marafiki kueleza namna walivyoguswa na kifo cha mmiliki wa kiwanda hicho, Bhaozang Ge maarufu Denis.

Mmiliki huyo wa kiwanda, raia wa China mwenye umri wa miaka 50, anadaiwa kuuawa usiku wa kuamkia Mei 16, 2026 ndani ya eneo la kiwanda hicho alikokuwa akiishi, huku tukio hilo likidaiwa kuhusisha walinzi binafsi wa kampuni hiyo. Inadaiwa pia walinzi hao waliondoka na begi lililokuwa na zaidi ya Sh10 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya malipo ya wafanyakazi na wauzaji wa makopo.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilithibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 19, 2026 na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika.

Akizungumza Mei 23, 2026 msibani hapo, mdogo wa marehemu, Baosheng Ge, amesema familia imepoteza mtu muhimu aliyekuwa nguzo kubwa ya msaada kwa ndugu, jamii na wafanyakazi wengi waliomtegemea.

Amesema tangu akiwa mdogo, marehemu alikuwa mtu mwenye bidii, aliyependa elimu na kazi, hali iliyomwezesha kujijengea maisha na baadaye kuwasaidia watu wengi.

“Alikuwa mtu mwenye juhudi, baada ya masomo alikuwa anarudi nyumbani kusaidia familia kufanya kazi za kilimo na shughuli nyingine za nyumbani,” amesema.

Baosheng amesema kaka yake alikuwa mtu mwenye moyo wa kipekee ambaye hakuwahi kuwatenga ndugu zake wakati wa shida na changamoto mbalimbali za maisha.

“Kwa kweli bila yeye baadhi yetu tusingefika hapa tulipo leo. Alitusaidia kupata kazi na kutusimamia katika maisha yetu ya kila siku,” amesema.

Aidha, amesema marehemu alikuwa akiamini katika usawa wa binadamu bila kujali tofauti za rangi au taifa.

“Alikuwa anasema binadamu wote ni sawa, tofauti iliyopo ni rangi tu. Hakupenda kabisa ubaguzi wa rangi,” amesema Denis.

Mbali na kusaidia familia, ndugu huyo amesema marehemu alikuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu wenye changamoto mbalimbali ikiwemo ada za shule na mahitaji muhimu ya maisha.

Mfanyakazi wa kampuni hiyo, Crispin Massawe, amesema amepokea kwa maumivu makubwa taarifa za kifo hicho kutokana na ukaribu aliokuwa nao na mwajiri wake tangu mwaka 2017.

“Nimeumizwa sana na msiba huu. Ijumaa kabla ya kifo chake nilimpa taarifa kuwa nimepata mtoto, akaniambia nije kesho nichukue zawadi. Lakini nilipofika nikakutana na taarifa za mauaji,” amesema Massawe kwa huzuni.

Naye Eveline Mhina amesema marehemu aliwahi kumpa mtaji wa Sh24 milioni ili aanzishe biashara bila hata kumlazimisha kurejesha fedha hizo baada ya biashara kushindwa.

“Bosi alikuwa na moyo wa kipekee. Niliposhindwa biashara hakunidai, badala yake aliniambia nirudi kiwandani kufanya kazi,” amesema.

Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku maarufu Musukuma, amesema tukio hilo linaacha maswali mengi na kuitaka Serikali pamoja na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ubainike.

“Dunia ya sasa ni kijiji, huyu mtu alikuwa kama Mtanzania kwa sababu ameishi hapa muda mrefu, alikuwa anaongea Kiswahili na alikuwa na marafiki wengi,” amesema Musukuma.

Amesema matukio ya aina hiyo yanaweza kuathiri taswira ya Tanzania kwa wawekezaji wa kigeni wanaokuja nchini kwa shughuli za biashara na uwekezaji.

“Hiki si kitendo kizuri kwa nchi yetu, Serikali inafanya kazi kubwa kuvutia wawekezaji. Matukio kama haya yanakatisha tamaa,” amesema.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Halmashauri ya Ubungo kutoka Idara ya Mazingira na Usafi, Grace Nnembuka, amesema marehemu alikuwa mshirika muhimu katika jitihada za utunzaji wa mazingira kupitia biashara ya ukusanyaji na uchakataji wa makopo.

“Tulikuwa tunashirikiana naye katika masuala ya mazingira. Sasa makopo yamekuwa na thamani kubwa tofauti na zamani yalivyokuwa yanaziba mitaro na kusababisha mafuriko,” amesema Grace.

Related articles

Recent articles