BOGOTA, Colombia
KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa Mei 31, 2026, Colombia imekuwa kwenye mfululizo wa matukio ya vurugu, yakihusisha pia kutekwa na hata kuuawa kwa wanasiasa.
Hali imekuwa mbaya zaidi maeneo ya Kusini mwa nchi hiyo, ambapo hivi karibuni msafara wa Seneta wa Chama Tawala, Alexander Lopez, alikumbana na vurugu na mwanasiasa huyo kunusurika kutekwa.
“Walijaribu kumteka Seneta,” alisema Rais wa Colombia, Gustavo Petro, ikikumbukwa kuwa Juni, 2025, Seneta mwingine, Miguel Uribe Turbay, aliuawa kwa kupigwa risasi ya kichwa akiwa katika mkutano wa kampeni.
Kwa mujibu wa Rais huyo, wahusika wa vurugu zinazoendelea katika maeneo mengi, hasa Kusini, ni magenge ya uhalifu wa biashara ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, kwa miaka mingi, Colombia imekuwa kwenye hali mbaya ya usalama kutokana na vurugu za jeshi la zamani (RAFC) na kundi la waasi la FARC.
Mwaka 2016, FARC walikaa mezani na Serikali na kukubaliana kumaliza vita lakini kwa miaka ya hivi karibuni kundi hilo limeamka na kurejesha usumbufu wake katika maeneo mbalimbali.


