MANCHESTER, Uingereza
BAADA ya kuifunga Chelsea bao 1-0, Manchester City si tu imetwaa ubingwa wa Kombe la FA, bali pia imeandika historia mpya kwenye michuano hiyo mikongwe katika soka la England.
Mechi ilichezwa Wembley na Man City walishuka dimbani wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza fainali mbili mfululizo za FA, wakifungwa na Man United na Crystal Palace.
Hilo ni taji la pili kwa Pep Guardiola msimu huu baada ya ubingwa wa Kombe la Ligi (EFL Cup) waliochukua kwa kuifunga Arsenal katika mchezo wa fainali.
Safari hii, ni Antoine Semenyo aliyefunga bao la dakika ya 72 na kuipa Man City taji msimu wa 145 wa Kombe la FA.
Man City ilifika fainali ikiwa imezifunga Exeter City, Salford City, Newcastle United, Liverpool na Southampton na ni taji lao la nane katika historia ya FA, sawa na Chelsea, Liverpool na Tottenham.
Kwa upande mwingine, Man City inakuwa timu ya kwanza katika historia ya soka la England kutwaa mataji mawili ya FA na EFL bila kupoteza mechi ndani ya msimu mmoja.
Chini ya Guardiola, Man City imefikisha vikombe 20 ya utumishi wa miaka 10 ya Mhispania huyo. Kwa FA, ni taji lake la tatu.
Pia, anakuwa kocha wa kwanza wa Ligi Kuu ya England kutwaa mara tatu au zaidi mataji ya FA (3), EFL (5) na Ligi ya Mabingwa Ulaya (3).
Kwa sasa, Man City wanarejesha hesabu zao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England, ambapo wamebakiza mechi mbili kumaliza msimu, huku wakiwa wameachwa pointi mbili na Arsenal iliyoko kileleni mwa msimamo.


