14 C
New York

Mwaka mmoja wa Papa Leo XIV ulivyobadili taswira ya Vatican

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

MWAKA mmoja baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, Mei 8, 202, ameendelea kuvuta hisia za dunia kwa mtindo wake wa uongozi, misimamo yake kuhusu haki za kijamii na uwezo wake wa kuunganisha utamaduni wa Marekani na Vatican.

Kuchaguliwa kwake mwaka jana kulivunja historia ya karne nyingi kwa kuwa Papa wa kwanza kutoka Marekani. Kabla ya hapo, wengi waliamini ilikuwa vigumu kwa Mmarekani kupewa nafasi hiyo kutokana na ushawishi mkubwa wa kisiasa wa taifa hilo duniani. Hata hivyo, ndani ya miezi 12, Leo XIV ameonyesha kuwa anataka kujulikana zaidi kama kiongozi wa kiroho kuliko mwanasiasa.

Tofauti na mtangulizi wake Papa Francis aliyekuwa akijulikana kwa kuvunja taratibu za Vatican, Leo XIV ameonekana kuwa mtulivu, mwenye kupima maneno na anayependa utaratibu. Lakini katika masuala ya haki za binadamu, uhamiaji, mazingira na amani duniani, ameendelea kufuata nyayo za Francis.

Katika mwaka wake wa kwanza, Papa Leo XIV ameonyesha wazi kutoridhishwa na namna wahamiaji wanavyotendewa nchini Marekani. Pia amepinga adhabu ya kifo na matumizi ya silaha za nyuklia. Msimamo huo umemweka katika mvutano wa wazi na Rais wa Marekani, Donald Trump, hasa baada ya Papa huyo kukosoa sera kali za uhamiaji.

Licha ya mvutano huo, watu wa karibu naye wanasema hajabadilika. Wanafafanua kuwa bado ni mtu mwenye ucheshi, anayependa mazungumzo ya kawaida na anayejali watu wa chini. Uzoefu wake wa kuhudumu nchini Peru katika maeneo yenye umaskini mkubwa umechangia sana mtazamo wake kuhusu usawa wa kijamii.

Papa Leo XIV pia ameleta sura mpya Vatican. Mara kadhaa ameonekana akiwa amevaa kofia ya timu ya baseball ya White Sox, kula pizza akiwa safarini na kuzungumza Kiingereza kwa lafudhi ya Marekani jambo lililomfanya kuwa karibu zaidi na vijana na jamii ya wanaozungumza Kiingereza duniani.

Katika masuala ya mageuzi ya Kanisa, Papa huyo ameonekana kuchukua hatua za taratibu badala ya kufanya mabadiliko ya ghafla. Ameendelea kuwapa wanawake nafasi kubwa ndani ya Vatican huku akisisitiza kuwa Kanisa linapaswa kuzungumzia zaidi haki, usawa na uhuru kuliko kujikita pekee katika mjadala wa masuala ya ngono.

Aidha, ameonyesha kuwa ni kiongozi anayeendana na teknolojia. Anatumia simu janja, saa za kidijitali na hata kuandika barua pepe mwenyewe, tofauti na ilivyozoeleka kwa viongozi wengi wa Vatican.

Katika mwaka mmoja tu, Papa Leo XIV ameonyesha kuwa ana dhamira ya kuijenga Vatican yenye sura ya kisasa lakini inayobaki na msingi wa kiroho. Kwa wengi, ameanza kuonekana si tu kama Papa wa kwanza kutoka Marekani, bali kama kiongozi anayejaribu kuunganisha dunia iliyogawanyika kupitia ujumbe wa amani, haki na mshikamano.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img