13.1 C
New York

WHO: Vita vya Iran ‘pasua kichwa’ sekta ya afya

Published:

TEHRAN, Iran

WIZARA ya Afya ya Iran imeeleza kuwa watu zaidi ya 1,300 wamefariki na wengine zaidi ya 9,000 kujeruhiwa tangu nchi hiyo ilipoingia kwenye vita na Marekani na Israel.

Kwa upande wa Lebanon, ambayo wapiganaji wake wa Hezbollah wanashambuliana na Israel, vifo ni 570 na majeruhi ni 1,400.

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) linalaani zaidi vitendo vya wapiganaji wa pande zote kuelekeza mashambulizi katika miundombinu ya afya katika nchi hizo.

Mathalan, WHO inaeleza kuwa vituo vya afya 18 nchini Iran vimeshambuliwa kwa mabomu tangu Februari 28, 2026, na kusababisha vifo nane vya wahudumu wa afya.

Kwa upande wa Lebanon, WHO imeeleza kuwa vituo vya afya 25 vimeshambuliwa, vikisababisha vifo 16 vya wahudumu wa afya na kujeruhi wengine 29.

“Katika machafuko ya aina yoyote, wafanyakazi wa afya, wagonjwa na vituo vya afya hulindwa na sheria za kimataifa,” imefafanua ripoti ya WHO.

Shirika hilo linaongeza kuwa watu zaidi ya 100,000 wamekimbia makazi yao nchini Iran, huku zaidi ya 700,000 wakifanya hivyo kwa upande wa Lebanon.

Kwa mujibu wa WHO, hali hiyo inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, kipindupindu, hasa kwa makundi ya watoto, wanawake na wazee.

Pia, kutokana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na moshi na kemikali za mabomu, WHO inaiona hatari ya kuibuka kwa magonjwa ya macho na ngozi.

Katika baadhi ya maeneo nchini Iran, Israel na Lebanon, vituo vya afya havifanyi kazi kabisa na vichache vilivyopo havina dawa za kutosha, kwa mujibu wa WHO.

Hivyo, Shirika hilo linazitaka pande zote zinazohusika katika mgogoro wa Mashariki ya Kati kuangalia namna ya kumaliza vita ili kuondosha ombwe lilipo kwenye sekta za afya.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img