22 C
New York

Makaa ya mawe injini mpya ya mageuzi ya viwanda

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema makaa ya mawe yana nafasi ya kimkakati katika kuharakisha mageuzi ya uchumi wa Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda. Amesema rasilimali hiyo si tu chanzo cha nishati, bali pia ni mhimili wa kuongeza thamani ya madini na malighafi nyingine za viwandani.

Akizungumza leo katika kikao na wadau wa sekta ya makaa ya mawe kilichofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Madini, jijini Dodoma, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya makaa ya mawe yanaweza kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, viwanda na madini.

“Makaa ya mawe ni mhimili muhimu katika maendeleo ya viwanda. Tunahitaji kuongeza uzalishaji na kuhakikisha matumizi yake yanaongeza thamani ndani ya nchi,” amesema Mavunde.

Katika kikao hicho, wachimbaji na wafanyabiashara wa makaa ya mawe walilalamika changamoto zinazohusiana na gharama za uzalishaji, usafirishaji na upatikanaji wa masoko. Waziri Mavunde ameahidi kuwa Serikali itazifanyia kazi changamoto hizo ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Aidha, amesisitiza kuwa upangaji wa bei elekezi utafanyika kwa ushirikishwaji wa wadau wote ili kulinda maslahi ya sekta.

Wadau wa makaa ya mawe wameipongeza hatua hiyo ya Waziri Mavunde, wakieleza kuwa ushirikishwaji wa wadau umeongeza imani na uwazi katika uendeshaji wa sekta. Pia wamesema wako tayari kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuongeza mapato ya Taifa kupitia Sekta ya Madini.

Ushirikiano na ushirikiano wa wadau

Katika kuimarisha mshikamano wa sekta, Mhe. Mavunde amewahimiza wadau kuanzisha chama chao (association) kitakachowaunganisha, kurahisisha shughuli zao na kushughulikia changamoto kwa pamoja kwa ufanisi zaidi.

Aidha, Waziri Mavunde amefichua kuwa Kampuni ya A1 Steels Tanzania LTD imepanga kujenga kiwanda cha kuzalisha chuma jijini Dodoma, ambacho kinatarajiwa kutumia takriban tani 20,000 za makaa ya mawe kwa mwaka. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuongeza mahitaji ya rasilimali hiyo, kuunda fursa zaidi za uzalishaji kwa wachimbaji wa ndani, kuongeza thamani ya madini na kuchochea ajira.

Kikao hicho kimeonesha dhamira ya Serikali ya kuifanya sekta ndogo ya makaa ya mawe kuwa injini ya maendeleo ya viwanda, huku ushirikiano kati ya Serikali na wadau ukiendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya sekta hiyo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img