12.6 C
New York

Watanzania 236 warejea nchini kutoka Dubai kwa ndege maalum ya ATCL

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WATANZANIA 236 mchana wa Machi 9, 2026 wamerejea nchini kwa ndege maalum ya Air Tanzania Company Limited baada ya kukwama mjini Dubai kwa muda kufuatia mvutano wa kijeshi unaoendelea kati ya Marekani, Israel na Iran.

ATCL imesema si kawaida kwa shirika hilo kupeleka ndege kubwa Dubai, lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa kuwasafirisha Watanzania waliokuwa wamekwama, ililazimika kufanya hivyo. Shirika hilo limeongeza kuwa linaweza kutuma ndege nyingine katika siku za karibuni endapo kutakuwa na uhitaji zaidi.

Afisa Uendeshaji Mkuu wa ATCL, Arif Jinnah, amesema safari hiyo haikuwa ya bure bali ilikuwa ya gharama nafuu ili kuwasaidia abiria waliokwama kurejea nyumbani. Aliongeza kuwa abiria wote waliopangwa kusafirishwa walifanikiwa kurejea, ingawa baadhi yao walilazimika kuacha mizigo yao.

Mashirika mengi ya ndege ya kimataifa yalisitisha safari kuelekea Mashariki ya Kati kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi baada ya Iran kuanza kulipiza kisasi dhidi ya hatua za Marekani na Israel.

Kutokana na hali hiyo, safari za ndege zinazoingia na kutoka katika viwanja vya ndege vya Tel Aviv, Dubai na Doha pamoja na vituo vingine vya kimataifa katika eneo hilo zimesitishwa kwa muda.

Iran imeripotiwa kufanya mashambulizi katika baadhi ya mataifa ya Ghuba kama sehemu ya kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyoanza mapema Jumamosi, Februari 28.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img