4.3 C
New York

A-Z mashambulizi ya Marekani, Israel kwa Iran

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

MAREKANI na mshirika wake mkubwa, Israel, zimeanzisha mashambulizi makubwa ya kivita dhidi ya Iran.

Milipuko ya mabomu imesikika katika miji mingi ya Iran, ikiwamo Isfahan, Qom, Karaj na Kermanshah.

Video zilizosambaa mitandaoni zinawaonesha raia wa Iran wakiwa na mfadhaiko, wasijue pa kukimbilia ili kujinusuru.

Licha ya kutokuwepo kwa taarifa rasmi juu ya majeruhi na vifo, inaelezwa kuwa tayari mashambulizi hayo yamekuwa yamesababisha watu 53 kupoteza maisha.

Trump ajigamba, Iran yajibu

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameiita operesheni hiyo kuwa ni maalumu kwa ajili ya kuishinikiza Serikali ya Iran isalimu amri.

“Muda mfupi uliopita, jeshi la Marekani lilianzisha operesheni yake nchini Iran,” alisema na kuongeza:

“Lengo letu ni kuwalinda watu wa Marekani kwa kuondosha vitisho vyote vinavyowekwa na utawala wa Iran.”

Awali, kabla ya kauli ya Trump, Waziri wa Ulinzi wa Israel alithibtisha nchi yake kuanza kuishambulia Iran.

Hatua ya Marekani na Iran kuishambulia Iran imekuja baada ya wiki kadhaa za kuitaka nchi hiyo kuacha uzalishaji wa silaha za nyuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameyaita mashambulizi hayo ya Marekani na Israel kuwa ni haramu na kinyume cha sheria.

Aidha, Araghchi alisema Iran itatumia njia zote za kiulinzi n kijeshi kujilinda dhidi ya muungano wa Marekani na Israel.

Katika hatua nyingine, Trump aliwataka raia wa Iran kubaki nyumbani wakati huu wa mashambulizi. “Tukimaliza (mashambulizi), chukueni Serikali yenu,” alisema.

UN, Uingereza, Ufaransa zatoa neno

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa kupitia Kitengo chake cha Haki za Binadamu kimezitaka pande zinazohusika kwenye mgogoro kukaa mezani kwa masilahi ya raia wa Iran.

Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja huo, Volker Turk, amesema: “Mara zote katika mgogoro wowote wa kivita, wanaoumia ni wananchi.”

Aidha, mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema kinachoendelea kinapaswa kuwalinda raia wa Iran na sheria za kimataifa.

Pia, Msemaji wa Serikali ya Uingereza, amesema: “Hatutaki kuona madhara makubwa zaidi. Kipaumbele chetu ni usalama wa raia wa Uingereza walioko huko (Iran na Mashariki ya Kati).

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema kilichotokea ni janga na mwendelezo wa hali mbaya ya usalama duniani.

“Mashambulizi yanayoendelea ni hatari kwa pande zote. Yanapaswa kukomeshwa. Ufaransa iko bega kwa bega kusimama na kuwalinda washirika wake,” amesisitiza.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, amesema nchi yake inaungana na Marekani na kuunga mkono hatua ya Iran kuzuiwa kuendelea na uzalishaji wa silaha za nyuklia.

Urusi yaibuka, yaziponda Marekani, Israel

Kwa upande wake, Serikali ya Urusi imelaani na kueleza kutokufurahishwa na kile kilichofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Katika taarifa yake, Urusi imetaka jumuhiya za kimataifa kuangalia na kuchukua hatua juu ya mashambulizi hayo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img