7.6 C
New York

Maajabu ya kitabu cha ‘Istilahi za Uhalifu na Usalama’

Published:

Na Christopher Cyrillo

FIKIRIA wewe ni mtumishi wa taasisi au mamlaka fulani ya kisiasa, na zaidi ya hapo wewe ni shushushu wa kuaminiwa na taasisi hiyo.

Mke wako anaugua saratani au ugonjwa mwingine hatari na nchini kwako hakuna huduma za afya za kiwango cha kumsaidia. Na taasisi unayoitumikia haipo tayari kugharamia matibabu ya mke wako nje ya nchi.

Mahasimu wenu wanagundua kuhusu ugonjwa wa mkeo na wanakuita na kukuambia wapo tayari kumsaidia gharama za matibabu nje ya nchi na kupona kabisa, lakini uwape siri za taasisi au mamlaka unayotumikia.

Je, utakubali kuuza nchi yako, taasisi yako au chama chako kwa ajili ya afya ya mkeo kipenzi?  Au utakataa ili uitwe ‘shujaa’ wa nchi yako, chama chako, au taasisi yako huku  mkeo akiendelea kuteseka na hatimaye kufa?

Hii ni mbinu ya kiitelijensia iitwayo Medi-Trap. Mashushushu wengi wamenaswa kwenye mtego huu na kujikuta wakivujisha siri nyeti za nchi zao ili wasaidiwe matibabu, wao wenyewe au ndugu zao wa karibu.

Nani anayeweza kuficha siri ya chama chake au nchi yake na kumuacha mke, mume, baba, mama au mtoto wake apoteze maisha?

Mwaka 1990 maafisa shirika la ujasusi la Israel (MOSSAD) waligundua kuwa mke wa Adnan Yasin, aliyekuwa afisa katika mamlaka ya Palestina (PLO) iliyokua na ofisi yake nchini Tunisia, anaumwa kansa na kwamba mumewe hakuwa na uwezo wa kumtibu.

Maafisa wa MOSSAD walimfuata Adnan na kumpa ‘ofa’ ya kugharamia matibabu ya mkewe katika hospitali kubwa nchini Ufaransa hadi apone kabisa lakini kwa masharti ya kuwapa siri za mamlaka ya Palestina (PLO).

Yani awe ‘double agent’. Adnan alipotafakari sana alikubali ‘ofa’ hiyo. Mkewe akapelekwa Ufaransa kwa matibabu na yeye akawa wakala wa kuvujisha siri za PLO kwa mashushushu wa MOSSAD.

Mke wa Adnan alilipiwa matibabu yake na wafanyabiashara wawili mjini Paris, ambao walijifanya wanatoa msaada (charity) lakini wakitumiwa na MOSSAD kwa siri.

Hatimaye Adnan akageuka kuwa ‘double agent’ wa MOSSAD na PLO kwa siri bila wapalestina wenzie kujua.

Wakati huo Adnan alikua Afisa kwenye ofisi ya Mahmoud Abbas maarufu kama Abu Mazen, ambaye alikua Mratibu wa shughuli za PLO kwenye makao makuu mjini Tunis, na Makamu mwenyekiti wa kamati kuu ya PLO. Alikua mtu mwenye nguvu kubwa kwa Wapalestina baada ya Yesser Arafat.

Adnan Yasin alifanya kazi kwenye ofisi ya Abu Mazen na pia alikua msaidizi (PA) wa balozi wa Palestina nchini Tunisia, Hakam Balawi. Kwahiyo alikua kwenye nafasi nzuri ya kujua siri nyingi za Palestina na kuzivujisha kwa MOSSAD.

Adnan alipewa vinasa sauti (tape recorder) na kutakiwa kuvipachika ndani ya ofisi ya Abu Mazen, bila kujulikana. Vinasa sauti hivyo viliundwa kwa teknolojia ya hali ya juu na haikua rahisi kugundulika.

Adnan aliviweka chini ya kiti cha Abu Mazen na kwenye taa ya mezani (table lamp) bila Abu Mazen kujua. Na viliweza kunasa mawasiliano mengi ya Abu Mazen bila kugundulika kwa kipindi cha miaka mitano (1990 – 1995).

Mwaka 1993 wakati wa mkataba wa Olso uliolenga kuwapatanisha Waisrael na Wapelestina ukiendelea huko nchini Norway, vinasa sauti hivyo vilikua kwenye ofisi ya Abu Mazen huku yeye akiwa ndiye mtia saini wa mkataba huo wa amani kwa upande wa Palestina.

Kwa sababu ya vinasa sauti hivyo, majasusi wa MOSSAD walifanikiwa kujua siri nyingi, mbinu na mipango ya Wapelestina dhidi ya Israel. Kwa sababu ya ‘kazi nzuri’ aliyowafanyia Waisrael, Adnan alipewa jina la ‘Golden Wool’ yani ‘sufu wa dhahabu’.

Mwaka 1993, Maafisa wa shirika la Ujasusi la Ufaransa (DGSE) waligundua kuwa mke wa Adnan analipiwa matibabu na watu wengine ambao si ndugu zake.

Kwa hiyo walifanya uchunguzi na kugundua kuwa gharama hizo zililipwa na maofisa MOSSAD, waliojifanya wafanyabishara na wasamaria wema.

Maafisa wa DGSE wakamhoji Adnan kuhusu matibabu ya mkewe na akakiri kushirikiana na MOSSAD kuvujisha siri za Palestina. Taarifa hiyo ikafanywa kuwa siri.

Lakini mawasiliano yaliyovujishwa na Adnan yaliwafanya MOSSAD kugundua pia makachero wengine ndani ya mamlaka ya Palestina waliokua wakitumiwa kuishughulikia Israel. Mmojawapo ni Atef Bseiso aliyekuwa shushushu wa ngazi za juu aliyetegemewa sana na Abu Mazen na Yasser Arafat.

Juni 8,1992 Bseiso aliuawa kwa kupigwa risasi na “watu wasiojulikana” mjini Paris. Hata hivyo Ufaransa ilitupiwa lawama kuhusika na mauaji hayo.

Tukio hilo liliwafanya maafisa wa DGSE wafanye uchunguzi wa kina na kugundua kuwa mauaji hayo yalifanywa na MOSSAD na kwamba Adnan ndiye aliyewapa MOSSAD taarifa zote muhimu kuhusu Bseiso hadi wakafanikiwa kumuua.

Ili kujisafisha kwamba haihusiki na mauaji hayo, Ufaransa ikabidi itoe siri. Shirika la Ujasusi la Ufaransa (DGSE) likaieleza mamlaka ya Palestina (PLO) kwamba mauaji hayo yalifanywa na MOSSAD na kwamba Adnan alikua ‘double agent’ aliyekua akivujisha siri za Palestina kwa Israel. Hivyo akatiwa nguvuni Oktoba 25, mwaka 1993 na kushtakiwa.

Soma mengi zaidi ndani ya kitabu cha ‘ISTILAHI ZA UHALIFU NA USALAMA’ kwa gharama ndogo ya TZS 30,000/=

Mawasiliano;  0713933736 au 0745830775

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img