10.5 C
New York

Upatikanaji wa umeme vijijini wachochea uchumi, RC Malima aipongeza REA

Published:

Na mwandishi wetu, Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na vitongojini, akisema hatua hiyo imechochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Malima ametoa pongezi hizo leo Februari 26, 2026, alipokutana na Bodi ya Nishati Vijijini (REB) pamoja na Menejimenti ya REA ofisini kwake, ambapo walifika kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme inayoendelea na iliyokamilika mkoani humo.

Amesema mafanikio yaliyofikiwa na REA yanapaswa kujivunia kutokana na mchango wake mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa umeme.

“Nimeifahamu REA kwa muda mrefu tangu ilipoanzishwa rasmi. Hapa ilipofika leo lazima tujivunie sisi kama Watanzania kwa kuwa imeweza kufikisha umeme katika vijiji vyote, na sasa utekelezaji unaendelea katika vitongoji vyote nchini,” amesema Malima.

Aidha, ameipongeza Bodi na Menejimenti ya REA kwa kusimamia kwa ufanisi miradi mbalimbali ya umeme katika mkoa huo, hatua inayowawezesha wananchi kunufaika na nishati hiyo muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, amesema REA itaendelea kutekeleza miradi ya umeme vijijini kwa weledi na kuhakikisha wakandarasi wanazingatia viwango na kukamilisha miradi kwa wakati.

“Sisi kama Bodi tuna uhakika miradi inayoendelea itakamilika kwa wakati, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha za kutosha kuwezesha utekelezaji wake,” amesema Kingu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy, amesema wakala huo unaendelea kupanua huduma ya umeme katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa, ambapo takribani maeneo 165 katika mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kunufaika na miradi mipya.

Ameongeza kuwa wateja wa awali 1,750 wanatarajiwa kuunganishiwa umeme kupitia miradi hiyo, huku Serikali ikitoa takribani Sh bilioni 7 kwa ajili ya utekelezaji wake mkoani humo.

Hatua hiyo inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme vijijini na vitongojini, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img