Na mwandishi wetu, Gazetini
SUALA la kupata nafasi ya ajira baada tu ya kumaliza masomo limekuwa ‘pasua kichwa’ kwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu. Si tu kwa Shahada (Degree), bali pia kwa Astashahada (Certificate) na Stashahada (Diploma).
Wakati hilo likizua mijadala mingi, yapo mambo ambayo yamekuwa yakitajwa kuchagiza uwepo wa ‘ukuta’ kati ya wahitimu na ajira.
Suala la ubora mdogo wa elimu wanayotoka nayo vyuoni, uwezo binafsi wa muhitimu na urasimu uliozaa rushwa na kujuana kwenye soko la ajira. Hayo ndiyo mambo matatu yanaozungumziwa zaidi.
Hata hivyo, Desemba, 2024, mtandao wa Intelligent.com ulifanya mahojiano na waajiri ili kupata mtazamo wao juu ya wahitimu waliowahi kuwafanyia usahili wa nafasi za kazi. Utafiti huo uliwafikia waajiri 1,000.
Asilimia 33 ya waajiri walisema wahitimu wapya hawana nidhamu ya kazi. Asilimia 24 walisema wahitimu wapya hawajaiva kumudu majukumu ya kazi.
Kwa upande mwingine, utafiti huo ulibaini kuwa mmoja kati ya wahitimu wapya wanne hufika kwenye chumba cha usahili wakiwa hawana maandalizi ya kutosha ya kukabiliana na maswali watayoulizwa na mwajiri.
Katika hilo, waajiri waliuambia mtandao wa Intelligent.com kuwa wahitimu wapya wengi wanakosa mbinu za kufauli usahili, nje ya uelewa mdogo wa maswali juu ya kazi/taaluma yao.
Mathalan, walitolea mfano uvaaji, kupatana juu ya mshahara na kukosa kujiamini, hasa katika eneo la kuwaangalia wanaomuuliza maswali wakati wa usahili.
Lakini pia, asilimia 23 ya waajiri walikiri kuwahi kukutana na matukio ya wahitimu wapya kufika chumba cha usahili wakiwa wamechelewa.
Asilimia 17 walisema wahitimu wapya, kwa maana ya wasio na uzoefu, wanaangushwa na uwezo mdogo wa stadi za mawasiliano.
Kwa upande wake, licha ya kukubaliana na utafiti, Mshauri wa masuala ya Elimu na Ajira, Huy Nguyen, anasema waajiri wanaweza kupata wafanyakazi wazuri kupitia wahitimu wapya endapo wataacha kujikita zaidi katika kutafuta uzoefu.
Wakati huo huo, Nguyen anawataka wahitimu wapya nao kuelewa dhana potofu iliyopo dhidi yao ili kujiweka katika nafasi ya kuajiriwa.
”Kwa kuelewa mambo yanayowakera waajiri, muhitimu anakuwa amejiongezea nafasi ya kuwazidi wengine katika maombi ya ajira,” anasema.


