RABAT, Morocco
YAKIWA ni maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2030, mbwa milioni tatu wameuawa nchini Morocco na kusababisha wanaharakati wa haki za wanyama kuibuka na kulaani kitendo hicho.
Morocco itashirikiana na Hispania na Ureno kuandaa michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kwa mujibu wa ripoti, mamlaka za Morocco zimeanza maandalizi, ikiwa ni pamoja na kuwaua mbwa wanaozurura mitaani kwa lengo la kuondosha kero kwa wageni watakaoingia kufuatilia mashindano hayo.
Wanaharakati wa haki za wanyama wamesambaza mitandaoni picha na video za mbwa waliokutwa na balaa hilo.
Aidha, wamelaani njia zinazotumika kuwaua mbwa hao kuwa ni pamoja na kuwakata shingo, kuwagonga na magari na kuwapa sumu.
Wakati huo huo, ripoti yao imeenda mbali zaidi na kuutaja Mji wa Marrakech kuwa ni kitovu cha mauaji ya mbwa hao.


