LONDON, Uingereza
KAMA kawaida, mechi za Ligi Kuu ya England (EPL) zitashuhudia mapumziko ya dakika kadhaa kuruhusu wachezaji watakaokuwa kwenye ibada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kupata chochote kitu cha kufungulia.
Ramadhan inatarajiwa kuanza wiki hii na itadumu kwa siku 29 au 30, ambapo waumini wa Kiislam hawatoruhusiwa kula wala kunywa hadi pale jua litakapozama.
Hivyo, kanuni ya mapumziko ya kupisha wachezaji waliofunga kufungulia yatakuwa kwa mechi za jioni.
Kama itakumbukwa, Kanuni hiyo ilitambulishwa na kuanza kutumika rasmi mwaka 2021.
Kwa mara ya kwanza, ilikuwa ni katika mchezo wa EPL uliozikutanisha Leicester City na Crystal Palace.
Katika mchezo huo, yalikuwepo mapumziko ya dakika 30, ambapo wachezaji Wesley Fofana na Cheikhou Kouyate walionekana wakifungulia.
Miongoni mwa wachezaji wa EPL wanaotarajiwa kuingia kwenye Mfungo wa Ramadhan msimu huu ni Mohamed Salah, William Saliba, Rayan Ait-Nouri na Amad Diallo.
Kwa baadhi ya klabu, zimeweza hata kufanya mabadiliko ya programu za mazoezi ili kuwasaidia wachezaji wao kukabiliana na ‘swaumu’.
Mwaka 2022, Sadio Mane akiwa Liverpool wakati huo, alisema klabu hiyo ilifanya hivyo.


