Na mwandishi wetu, Gazetini
WANAWAKE takribani 500,000 waliacha kazi nchini Marekani, kwa mujibu wa takwimu za Jarida la Forbes. Takwimu hizo ni kuanzia Januari hadi Oktoba, 2025.
Wakati Marekani ikipata anguko kubwa hilo, Afrika imeshuhudia wanawake wakichomoza na kufanya makubwa katika tasnia mbalimbali.
Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, hawa ni wanawake sita wenye mvuto mkubwa kutokana na mfanikio yao barani Afrika.
Mary Vilakaz (Afrika Kusini)
Alizaliwa Agosti, 1977. Ni mfanyabiashara mkubwa huko Afrika Kusini. Amekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya fedha nchini humo.
Kwa sasa, Vilakaz ni mmoja ya watu ‘wazito’ katika Kampuni ya FirstRand. Hiyo ndiyo kampuni ya masuala ya kifedha yenye thamani kubwa zaidi nchini humo.
Judith Suminwa Tuluka (DRC)
Ni mchumi na mwanasiasa maarufu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Mwaka 2024, aliandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Waziri Mkuu nchini humo.
Kabla ya nafasi nyeti hiyo, Tuluka alikuwa mwajiriwa wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Aliwahi pia kuwa Waziri wa Mipango katika utawala uliopita.
Netumbo Nandi-Ndaitwah (Namibia)
Mwanasiasa na mwanadiplomasia mwenye ushawishi mkubwa nchini Namibia. Marchi 21, 2025, alichaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Taifa hilo.
Kabla ya kuingia Ikulu, Nandi-Ndaitwah wa Chama kilichopigania uhuru, SWAPO, aliwahi kuwa Waziri wa Mazingira na Utalii, Waziri wa Mambo ya Nje, Naibu Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.
Mpumi Madisa (Afrika Kusini)
Madisa ni mtaalamu wa masuala ya bima nchini Afrika Kusini. Alipoajiriwa na kampuni ya Bidvest mwaka 2003, alianzia ngazi mbalimbali za chini.
Baada ya kuhudumu katika nafasi nyingi, ikiwamo ya Mkurugenzi wa Masoko, sasa Madisa ndiye Mkurugenzi Mtendaji (CEO) na Bidvest ni moja ya kampuni bora 40 za bima nchini Afrika Kusini, ikiwa na wafanyakazi takribani 130,000.
Ngozi Okonjo-Iweala (Nigeria)
Mtaalamu wa uchumi na uandaaji wa sera. Mwaka 2010, alisimamia harambee ya Benki ya Dunia iliyokusanya Dola bilioni 49.3 zilizotumika kuzipa mikopo nchi masikini.
Kwa sasa, Okonjo-Iweala ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara la Kimataifa, akiwa ni mwanamke wa kwanza wa Afrika kuteuliwa kukalia kiti hicho.
Mo Abudu (Nigeria)
Ni mfanyabiashara anayemiliki vyombo vya habari nchini humo. Ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya EbonyLife Media inayomiliki vituo vya runinga na vyombo vingine vya habari.
Mwaka 2025, Abudu alitajwa na Jarida maarufu la TIME kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.


