10.5 C
New York

Visual| Makocha bora 10 wa muda wote EPL

Published:

LONDON, Uingereza

KWA miaka zaidi ya 33, Ligi Kuu ya England (EPL) imeshuhudia makocha wakiingia na kutoka, wachache tu wakimudu ushindani uliopo na kujijengea heshima kubwa.

Makala haya yanakuibulia na kuchambua makocha 10 walioweza kujenga ufalme wao katika Ligi hiyo inayotajwa kuwa na wafuatiliaji wengi zaidi duniani.

Alex Ferguson

Historia ya EPL haiwezi kukamilika bila kumtaja ‘Fergie’, ambaye ni kocha wa kwanza kubeba mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu hiyo.

Hadi anaondoka Manchester United mwaka 2003, kocha huyo raia wa Scotland alikuwa na mataji 13 ya EPL kwa miaka 26 aliyoinoa timu hiyo.

Pep Guardiola

Baada ya miaka mingi ya Wenger na Alex Ferguson kutamba EPL, Guardiola ndiye anayefanya hivyo kwa sasa. Amebeba mara sita ubingwa wa EPL ndani ya misimu tisa tu iliyopita.

Msimu wa 2022-23 ulikuwa wa mafanikio zaidi, ambapo aliiongoza Manchester City kubeba mataji matatu kwa mpigo, likiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Arsene Wenger

Mwaka 1998, ‘Profesa’ aliweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa kigeni kutwaa mataji mawili kwa mpigo katika soka la England.

Msimu wa 2003-04, aliiwezesha Arsenal kutwaa ubingwa wa EPL bila kufungwa, akiwa kocha wa kwanza kufanya hivyo baada ya miaka 115. Aliondoka klabuni hapo akiwa amehudumu kwa miaka 22.

Jose Mourinho

Katika miaka ya 2000, ‘Special One’ alizivuruga Arsenal na Manchester United kwa kutwaa mataji mawili mfululizo ya EPL akiwa na Chelsea. Alibeba tena msimu wa 2014-15.

Akiwa England, pia kocha huyo wa kimataifa wa Ureno aliwahi kufanya kazi na klabu za Manchester United na Tottenham.

Jurgen Klopp

Mjerumani huyo anatajwa kuwa ndiye kocha bora kuwahi kutokea Liverpool tangu enzi za Bill Shankly na Bob Paisley.

Klopp, kocha wa zamani wa Borussia Dortmund, atakumbukwa kwa kuipa Liverpool taji la kwanza la EPL baada ya ukame wa miaka zaidi ya 30.

David Moyes

Aliifanya Everton kuwa tishio EPL kwa miaka 11 aliyokaa kwenye benchi. Aliiwezesha kuingia kwa mara ya kwanza ‘Top Four’ msimu wa 2004-05.

Ni mafanikio hayo ndiyo yaliyoisukuma Manchester United kumpa nafasi ya kuchukua mikoba ya Alex Ferguson, ingawa hakuweza kuirejesha timu hiyo kwenye ubora wake.

Claudio Ranieri

Aliajiriwa na Leicester City msimu wa 2025-16 na huo ukawa msimu wake mzuri wa kuipa taji la Ligi Kuu ya England kwa mara ya kwanza katika historia.

Hata hivyo, haikuwa mara ya kwanza kwa Ranieri kufanya kazi EPL. Alikuwa kocha wakati Chelsea iliposhika nafasi ya pili msimu wa mwisho kwa Arsenal kutwaa ubingwa wa EPL. Ni msimu wa 2003-04.

Carlo Ancelotti

Alitua Chelsea mwaka 2009 akitokea AC Milan na kutwaa taji la EPL katika msimu wake wa kwanza tu Stamford Bridge.

Chini yake, Chelsea ilibeba taji na kuweka rekodi ya kuwa timu iliyofunga mabao mengi (103) ya msimu mmoja katika historia ya EPL.

Harry Redknapp

Hakuwahi kutwaa ubingwa wa EPL kwa miaka zaidi ya 20 aliyofanya kazi ya ukocha lakini aliiwezesha West Ham United kushiriki Ligi Kuu hiyo.

Hata hivyo, atakumbukwa zaidi kwa kazi kubwa aliyoifanya Tottenham, ambapo aliweza kuwa Kocha Bora wa EPL msimu wa 2009-10, licha ya timu hiyo kukosa ubingwa.

Roberto Mancini

Muitalia huyo ndiye kocha wa kwanza kuipa Manchester City ubingwa wa EPL. Aliajiriwa mwaka 2009 kuchukua nafasi ya Mark Hughes na kutwaa taji la FA misimu miwili tu baadaye.

Mancini aliondoka kwa heshima Man City akiwa na rekodi nzuri ya kushinda asilimia 62 ya mechi alizokaa klabuni hapo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img