BEIJING, China
IDADI ya watoto waliozaliwa mwaka 2025 nchini China ni ndogo zaidi kuwahi kutokea katika Taifa hilo la Asia.
Ni kwa mwaka wa nne mfululizo sasa China imeshuhudiwa ikiporomoka katika idadi ya watoto wanaozaliwa.
Hiyo ni licha ya Serikali ya China kuendeleza kampeni za kuhamasisha vijana kuoa ili kupata watoto.
Hivi karibuni, Serikali ilitangaza zawadi ya kitita cha Dola 375 hadi 500 kwa wazazi wenye watoto wa umri wa chini ya miaka mitatu.
Kwa wataalamu wa uchumi, kushuka kwa idadi ya watoto wanaozaliwa kutaathiri shughuli za maendeleo, hivyo jitihada zaidi zinahitajika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu mpya za Serikali, kiwango cha kuzaliana kwa raia wa China kimeshuka kwa asilimia 5.63, kikiwa ni kiwango kikubwa zaidi. Wakati huo huo, kile kilichooneshwa katika takwimu hizo ni kwamba idadi ya vifo imeongezeka kwa asilimia 8.04.
Aidha, kiwango hicho cha vifo ni kikubwa zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 1968. Ikumbukwe, China inatajwa kuwa na watu bilioni 1.4, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025.


