Na mwandishi wetu, Gazetini
MALARIA imeendelea kuwa changamoto kubwa barani Afrika, huku mataifa ya Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya (DRC), Niger na Tanzania yakitajwa kuteswa zaidi na ugonjwa huo.
Ripoti ya Mwaka huu ya Malaria, ambayo imehusisha takwimu kutoka mataifa 80, inachambua ukubwa wa changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, malaria imehusika kwa asilimia zaidi ya 50 katika vifo vinavyotokea katika mataifa manne hayo.
Nigeria inaongoza ikiwa na vifo 185,000 vitokanavyo na malaria. Ni asilimia 30.3 ya vifo vya malaria duniani kote. Miongoni mwa sababu ni kukosekana kwa programu madhubuti za kukabiliana na ugonjwa huo.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa DRC inafuata ikiwa na vifo 68,000, sawa na asilimia 11.1, hiyo ikitokana na sababu mbalimbali, ikiwamo miundombinu mibovu ya huduma za afya.
Niger na Tanzania, kama zilivyotajwa awali, nazo ziko kwenye janga hilo. Wakati Niger ikiwa na vifo 35,000 (5.8%), Taifa hilo la Afrika Mashariki lina 26,000 (4.3%).
Hata hivyo, Afrika imeshuhudia mafanikio makubwa katika kukabiliana na malaria. Mwaka 2024, jitihada mbalimbali, zikiwamo kampeni za kuhamasisha matumizi ya vyandarua, zilizuia maambukizi milioni 170 na kuokoa vifo milioni moja.
Kufikia Oktoba, 2025, mataifa 24 ya Afrika yalikubali chanjo ya malaria kuingia katika programu za kinga zao. Pia, mataifa ya Cape Verde na Misri yalitangazwa kuwa yametokomeza kabisa ugonjwa huo.
Takwimu za ujumla zinaonesha kuwa malaria ni chanzo cha vifo zaidi ya milioni 280 duniani kote. Takwimu hizo ni za mwaka 2024, hivyo huenda idadi imeongezeka au kupungua.


