10.7 C
New York

‘Ndoa ya Xabi Alonso na Real Madrid yavunjika’

Published:

MADRID, Hispania

KLABU ya Real Madrid ya Hispania leo Jumatatu, Januari 12, 2026, imethibitisha kuachana na kocha wake mkuu, Xabi Alonso, baada ya pande zote kufikia makubaliano ya kusitisha ushirikiano wao.

Alonso, aliyekuwa kiungo mahiri wa zamani wa klabu hiyo, anaondoka Bernabéu baada ya kuitumikia timu kwa zaidi ya miezi saba tangu ateuliwe rasmi kushika mikoba hiyo Juni 1 mwaka jana. Uamuzi huo umefikiwa siku moja baada ya Madrid kupoteza fainali ya Kombe la Supercopa kwa mabao 3-2 dhidi ya hasimu wao wakubwa, Barcelona.

Mbali na kipigo hicho, hali ya ushindani katika La Liga pia imechangia maamuzi hayo, ambapo Real Madrid kwa sasa iko nyuma kwa pointi nne dhidi ya Barcelona wanaoongoza msimamo wa ligi.

Alonso aliwasili Madrid akiwa na sifa kubwa kufuatia mafanikio yake makubwa akiwa Bayer Leverkusen, ambako aliipa klabu hiyo mataji mawili ya ndani msimu wa 2023–24 na kuifikisha fainali ya Ligi ya Europa. Mwanzo wake Santiago Bernabéu ulikuwa wa kuvutia, akifanikiwa kushinda mechi 13 kati ya 14 za awali, isipokuwa kipigo kizito cha dabi dhidi ya Atlético Madrid.

Hata hivyo, hali ilianza kubadilika baada ya kipigo dhidi ya Liverpool Novemba 4, 2025, kilichoanzisha mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha, ambapo Madrid ilishinda mechi mbili tu kati ya nane. Ingawa baadaye Alonso alirejesha matumaini kwa kushinda mechi tano mfululizo, viongozi wa klabu waliamini hilo halikutosha kuendelea kumpa imani ya muda mrefu.

Katika taarifa rasmi, Real Madrid ilieleza kuwa: “Kwa makubaliano ya pande zote kati ya klabu na Xabi Alonso, imeamuliwa kumaliza kipindi chake kama kocha mkuu wa timu ya kwanza.

Xabi Alonso ataendelea kuheshimiwa na kupendwa na Madridistas wote, kwani ni gwiji wa klabu hii na amekuwa akiishi na kutetea maadili ya Real Madrid. Klabu hii daima itabaki kuwa nyumbani kwake.”

Klabu hiyo pia ilimshukuru Alonso pamoja na benchi lake la ufundi kwa kazi na kujitolea walikoonesha, huku ikiwatakia mafanikio mema katika hatua inayofuata ya taaluma zao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nafasi ya Alonso itachukuliwa kwa muda na nyota wa zamani wa Real Madrid, Álvaro Arbeloa, ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya vijana ya klabu hiyo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img