Na mwandishi wetu, Gazetini
KILA ifikapo Desemba ya kila mwaka, maandalizi na shamrashamra za Sikukuu ya Krismas huonekana wazi katika maeneo mengi duniani.
Tofauti na miezi mingine, siku chache kuelekea Desemba 25 hupambwa na miti ya Krismas na hata mijumuhiko ya familia katika jamii nyingi.
Hata hivyo, ni maeneo mengi lakini siyo yote duniani husherehekea Krismas kila ifikapo siku hiyo. Sikukuu ya Krismas huwa haiwi siku moja katika mataifa yote duniani.
Kwamba licha ya Desemba 25 kuwa Sikukuu ya Krismas katika mataifa mengi ya Ulaya, yapo yanayosherehekea Januari 7. Takribani wiki mbili baada ya wenzao.
Iko hivi; kwa mataifa yanayoitambua Desemba 25 kuwa ndiyo Krismas, yanaifuata kalenda ya Gregoria iliyoasisiwa na Papa Gregory XIII mwaka 1582.
Kwa tamaduni za Wakiristo wa Ulaya ya Magharibi, wakiwamo Wakatoliki na mengi miongoni mwa makanisa ya Anglikana, wanaifuata kalenda hiyo wakiamini Desemba 25 ndiyo siku aliyozaliwa Yesu.
Ni tofauti na tamaduni za Wakiristo wa Ulaya ya Mashariki na Kusini-Mashariki mwa Ulaya, kwa maana ya Urusi, Serbia, Montenegro, North Macedonia, na baadhi ya maeneo ya Ukraine na Georgia.
Kwao, Sikukuu ya Krismas ni Januari 7 ya kila mwaka. Katika maeneo hayo, kalenda inayotumika ni ile ya Julian, ambayo iko mbele ya ile ya Gregoria kwa siku 13.
Lakini pia, zipo baadhi ya nchini hapa duniani, ikiwamo Uturuki, ambazo zinaendeshwa kwa misingi ya Dini ya Uislam, hivyo haziitambui Krismasi kuwa ni Sikukuu maalumu katika mipango ya Serikali.
Mathalan, haiwezi kusababisha mapumziko ya watumishi wa Serikali na kuathiri kwa namna yoyote ile shughuli za kila siku.


