10.5 C
New York

Makocha ‘walioifilisi’ Chelsea baada ya kutimuliwa

Published:

LONDON, Uingereza

BAADA ya kuvunja mkataba wake, Chelsea wamelazimika kumlipa Enzo Maresca kitita cha Pauni milioni 10, kwa mujibu wa Gazeti la Sun.

Kocha huyo raia wa Italia, alifutwa kazi siku chache zilizopita akiwa amehudumu kwenye benchi la ufundi kwa kipindi cha miezi 14 pekee.

Hata hivyo, si jambo geni kwa Chelsea. Kuna orodha ndefu ya makocha waliochota fedha nyingi kama fidia ya kuvunjiwa mkataba na klabu hiyo ya jijini London.

Antonio Conte (Chelsea)

Chelsea ilimuajiri mwaka 2016. Aliwapa taji la Ligi Kuu ya England msimu wake wa kwanza tu pale Stamford Bridge.

Msimu uliofuata (2017-18) haukuwa mzuri. Blues waliumaliza katika nafasi ya tano na hapo ukaibuka mgogoro mkubwa kati yake na mabosi wa Chelsea.

Alipovunjiwa mkataba, mabosi wa Chelsea walilazimika kumlipa Muitalia huyo kiasi cha Pauni milioni 26.2.

Jose Mourinho (Chelsea)

Akiwa na mafanikio makubwa klabuni hapo, mataji sita kwa miaka mitatu, Mourinho aliondoka Chelsea mwaka 2007. Zipo taarifa kuwa baadhi ya wachezaji walilia. Aliondoka kutokana na uhusiano wake mbaya na uongozi.

Hakuondoka bure. Kitendo cha Blues kumvunjia mkataba kilimfanya ‘Special One’ kuchota kitita cha Pauni milioni 18.

Luis Felipe Scolari (Chelsea)

Chelsea walimpa ajira mwaka 2008 lakini alidumu klabuni hapo kwa miezi nane pekee. Akatimuliwa.
Hata hivyo, bingwa huyo wa Kombe la Dunia mwaka 2002 akiwa kocha wa timu ya taifa ya Brazil, alilipwa Pauni milioni 13.6 kwa kuvunjiwa mkataba.

Thomas Tuchel (Chelsea)

Kocha huyo wa kimataifa wa Ujerumani alifukuzwa Stamford Bridge ukiwa umebaki mwezi mmoja tu kabla ya kuanza kwa msimu wa 2022-23.

Tuchel, ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya England, alilipwa Pauni milioni 13 kwa kuvunjiwa mkataba na Chelsea.

Graham Potter (Chelsea)

Aliajiriwa kuchukua nafasi ya Tuchel. Ni baada ya kazi nzuri aliyoifanya kocha huyo raia wa England akiwa mkuu wa benchi la ufundi la Brighton.

Potter alianza vizuri kwa kushinda mechi sita kati ya 11 lakini alidumu Chelsea kwa miezi nane tu. Akafungashiwa virago, ingawa alilipwa Pauni milioni 13.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img