Na mwandishi wetu, Gazetini
DUNIA imewahi kushuhudia matukio mengi ya waandamanaji wakipinga viongozi na hata serikali zao pale walipoona mambo hayaendi kama wanavyotaka au walivyotarajia.
Lakini, kile kilichowahi kutokea katika maandamano ya mwaka 1672 nchini Uholanzi ni zaidi ya tafsiri ya ‘wananchi wenye hasira kali’. Ilikuwaje?
Makala ya historia iliyochapishwa katika mtandao wa World Visualized inasimulia tukio hilo la kusisimua ikianza hivi;
Mwaka 1672, yalizuka maandamano makubwa nchini Uholanzi, ambapo wananchi waliingia barabarani mjini Hague kulalamikia mambo kadhaa.
Chini ya Johan de Witt, ambaye kwa sasa ni kama Waziri Mkuu, Uholanzi ilikuwa ikipitia changamoto kadhaa, ikiwamo ya hali mbaya ya kiuchumi.
Hasira za wananchi zilielekea kwa De Witt, ingawa inaelezwa kuwa zilichochewa na propaganda za wakosoaji wake wa ndani.
Hatimaye, waandamanaji walifanikiwa kumkamata De Witt na kaka yake, Cornelis, na kuwachoma moto, kisha kula baadhi ya viungo vya mwili wa kiongozi huyo.
Leo hii, licha ya ustawi wa demokrasia nchini Uholanzi, bado kitendo hicho kinatajwa kubaki kama alama ya ‘hasira za wananchi’ dhidi ya serikali iliyoshindwa kufikia matarajio ya wengi.


