Na mwandishi wetu, Gazetini
MAFUNZO ya kikanda Nairobi yawezesha wawakilishi kutoka nchi tisa za Afrika kuandaa mipango ya biashara na mapendekezo ya uwekezaji yanayolenga kukabiliana na uharibifu wa ardhi na kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za asili.
Mashirika ya kiraia barani Afrika yameimarisha uwezo wa kuhamasisha uwekezaji na kupata ufadhili kwa ajili ya kurejesha ardhi iliyoharibika, kufuatia mafunzo ya kikanda yaliyolenga kuwajengea washiriki ujuzi wa kuandaa mipango ya biashara na mapendekezo ya uwekezaji yenye uwezo wa kuvutia fedha.
Mafunzo hayo ya siku tatu yalifanyika katika Karen Country Club jijini Nairobi, Kenya, kuanzia Juni 26 hadi 28, 2026, chini ya mradi wa Kuimarisha Nafasi ya Mashirika ya Kiraia katika Kufanikisha Lengo la Kutokuwa na Upotevu wa Ardhi (CS4LDN).
Mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na kutekelezwa na Taasisi ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), kwa ushirikiano na Drynet pamoja na Both ENDS.
Mafunzo hayo yaliwakutanisha wawakilishi 16 wa mashirika ya kiraia kutoka Burkina Faso, Cameroon, Ethiopia, Ghana, Kenya, Mali, Senegal, Sudan Kusini, Tanzania na Zambia, kwa lengo la kuimarisha mchango wao katika urejeshaji wa ardhi, usimamizi endelevu wa mifumo ya ikolojia na mapambano dhidi ya uharibifu wa ardhi.

Ufadhili, kikwazo katika urejeshaji wa ardhi
Licha ya mashirika ya kiraia kuwa na nafasi muhimu katika kushirikiana na jamii na kuendeleza uhifadhi wa mazingira, upatikanaji mdogo wa rasilimali za kifedha unaendelea kuwa kikwazo kwa utekelezaji na upanuzi wa miradi ya urejeshaji wa ardhi.
Mafunzo hayo yalilenga kuziba pengo hilo kwa kuwapa washiriki ujuzi wa vitendo wa kuandaa mipango ya biashara na mapendekezo ya uwekezaji yanayotekelezeka kifedha, kutambua fursa za ufadhili, kushirikiana na wafadhili watarajiwa na kusimamia rasilimali kwa ufanisi.
Katika vipindi vya mafunzo shirikishi, washiriki walijadili changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa fedha katika nchi zao, wakabadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kuandaa mapendekezo yanayokidhi vipaumbele vya wafadhili huku yakionesha manufaa yanayoweza kupimika kwa mazingira na jamii.
Mafunzo pia yalisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji, usawa wa kijinsia na matumizi ya mbinu zinazozingatia mifumo ya ikolojia katika kubuni na kutekeleza miradi ya Lengo la Kutokuwa na Upotevu wa Ardhi (LDN).
Kuunganisha uhifadhi na uwekezaji
Mafunzo hayo yalijengwa juu ya matokeo ya ripoti ya mradi wa CS4LDN yenye kauli mbiu Kufungua Fursa za Ufadhili kwa Ajili ya Kutokuwa na Upotevu wa Ardhi (Unlocking Finance for Land Degradation Neutrality).
Ripoti hiyo inachambua changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha LDN na kupendekeza mbinu za kuimarisha ushirikiano kati ya wafadhili na mashirika ya kiraia. Ripoti inapatikana kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kihispania.
Lengo la LDN ni kuhakikisha kuwa kiasi na ubora wa rasilimali za ardhi vinabaki thabiti au vinaongezeka kwa muda, kupitia kuzuia uharibifu wa ardhi, kusimamia ardhi kwa njia endelevu na kurejesha maeneo yaliyoharibika.
Uwekezaji katika juhudi hizo unaweza kuchangia kulinda rutuba ya udongo, kuimarisha mifumo ya ikolojia na kusaidia maisha ya jamii zinazotegemea kilimo na rasilimali za asili. Hata hivyo, kufikia matokeo hayo kunahitaji miradi yenye mipango thabiti, uendelevu wa kifedha na ushirikishwaji wa jamii husika.
Mfumo wa ulezi kuendeleza maarifa
Mbali na kuongeza ujuzi wa kuandaa mapendekezo ya uwekezaji, mafunzo hayo yalitoa fursa ya kujenga mitandao ya kikanda na kuimarisha ushirikiano kati ya mashirika yanayofanya kazi katika urejeshaji wa ardhi na uhifadhi wa mazingira.
Washiriki walikubaliana kuendeleza maarifa yaliyopatikana kwa kutumia mfumo wa ushauri na ulezi wa kitaalamu (mentorship), ambapo kila shirika litasaidia angalau shirika jingine au mshiriki mmoja kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa ujuzi uliopatikana hauishii kwa washiriki waliohudhuria mafunzo pekee, bali unasambaa kwa mashirika mengine na kuongeza uwezo wa pamoja wa kutafuta fedha na kutekeleza miradi yenye manufaa kwa mazingira.
Mradi wa CS4LDN unalenga kuimarisha uwezo wa mashirika ya kiraia duniani kushawishi na kuchangia utekelezaji wa sera na uwekezaji unaosaidia kufanikisha LDN. Ukiungwa mkono na Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa (UNCCD) pamoja na Jopo la Mashirika ya Kiraia, mradi huo unaunganisha hatua za jamii na michakato ya sera na ufadhili katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Mafunzo ya Nairobi yanaweka mkazo katika umuhimu wa kuunganisha juhudi za uhifadhi na mikakati ya upatikanaji wa fedha, ili mashirika ya kiraia yaweze kubadilisha mipango ya kurejesha ardhi kuwa miradi inayotekelezeka, yenye matokeo yanayopimika na manufaa ya muda mrefu kwa mazingira na jamii.


