Na mwandishi wetu, Gazetini
WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umewahamasisha waajiri nchini kuwekeza katika usalama na afya za wafanyakazi kwa kuimarisha uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuanzisha programu endelevu za mazoezi katika maeneo ya kazi.
Wito huo umetolewa wakati wa Bonanza la Waajiri lililofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lililoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), ambapo OSHA ilishiriki kama mdhamini na kutoa elimu kuhusu usalama na afya mahali pa kazi.
Akizungumza katika bonanza hilo, Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Dk. Evaline Munisi, amewapongeza viongozi wa ATE kwa kuandaa tukio lililowakutanisha waajiri na wafanyakazi kupitia michezo na shughuli za kuimarisha afya.
Amesema bonanza hilo limetoa fursa kwa waajiri kujifunza mbinu za kujenga mazingira salama ya kazi kupitia elimu na huduma za uchunguzi wa afya za wafanyakazi zilizotolewa sambamba na shughuli za michezo.
“Ninawasihi waajiri wote kulifanya suala hili la afya na ustawi wa wafanyakazi kuwa sehemu ya mikakati yenu ya kibiashara badala ya kulichukulia kama tukio la siku moja,” amesema Dk. Munisi.
Ameongeza kuwa waajiri wanapaswa kuwekeza katika uchunguzi wa afya wa mara kwa mara na kuweka programu endelevu za mazoezi mahali pa kazi ili kusaidia kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha afya ya akili na kuboresha usalama na afya kazini.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran, amesema chama hicho kinaendelea kushirikiana na OSHA kuhamasisha uzingatiaji wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, hatua inayolenga kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuongeza tija katika uzalishaji.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa waajiri kuweka mikakati ya kulinda afya za wafanyakazi, ikiwemo kuanzisha programu za michezo na kuhakikisha wanapata huduma za uchunguzi wa afya mara kwa mara.
Mbali na kutoa elimu kwa washiriki, OSHA ilishiriki michezo mbalimbali iliyojumuisha netiboli, kuvuta kamba, mbio fupi, voliboli na kukimbia ndani ya magunia.
Katika mashindano hayo, OSHA ilishika nafasi ya kwanza katika michezo ya kuvuta kamba, mbio fupi na kukimbia ndani ya magunia, huku ikipata nafasi ya pili katika netiboli na voliboli.


