11.9 C
New York

Mikataba ya zabuni za makundi maalum yafikia Sh bilioni 74.32

Published:

*Makamu wa Rais, Waziri waisifu PPRA kwa kuwezesha vijana

Na mwandishi wetu, Gazetini-Rukwa

Makundi maalum ya Watanzania yamepata mikataba 3,466 ya zabuni za umma yenye thamani ya Sh bilioni 74.32 katika kipindi cha Julai 2023 hadi Oktoba 13, 2026, huku vijana wakiongoza kwa idadi ya mikataba na thamani ya fedha walizopata.

Takwimu hizo ziliwasilishwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, katika ripoti ya mbio hizo zilizohitimishwa Oktoba 14, 2026.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa jumla ya makundi 33,524 ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu yalisajiliwa katika mfumo wa ununuzi wa umma na kupata fursa za mikataba ya zabuni.

Katika kundi la vijana, mikataba 2,066 yenye thamani ya Sh bilioni 40.56 ilipatikana, huku wanawake wakipata mikataba 1,264 yenye thamani ya Sh bilioni 29.76.

Kwa upande mwingine, wazee walipata mikataba 93 yenye thamani ya Sh bilioni 3.36, huku watu wenye ulemavu wakipata mikataba 43 yenye thamani ya Sh milioni 635.7.

Akizungumza katika hotuba ya kufunga Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, aliipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kuweka mifumo inayowezesha makundi hayo kushiriki katika zabuni za Serikali.

“Ninaisifu sana PPRA kwa hatua kubwa na za mfano walizochukua katika kuwezesha fursa za ununuzi wa umma kwa wananchi wetu.

“Kuona kwamba zaidi ya makundi 33,500 ya wananchi yamesajiliwa na kupata fursa za mikataba ya zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 74.32 ni ushahidi thabiti kuwa Serikali inafanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote,” alisema Ndejembi.

Naye Waziri mwenye dhamana ya vijana, Joel Nanauka, alisema mikataba iliyopatikana na vijana inaonesha nafasi ya ununuzi wa umma katika kufungua fursa za kiuchumi kwa kundi hilo.

“Vijana ndio nguvu kazi kuu ya taifa hili. Ripoti za ununuzi wa umma zilizosimamiwa na PPRA zinaonesha wazi jinsi milango ya fursa ilivyofunguka.

“Zaidi ya mikataba 2,000 yenye thamani inayozidi Sh bilioni 40 imekwenda mikononi mwa vijana wetu. Hili ni fanikio kubwa mno linalostahili pongezi za dhati,” alisema Nanauka.

Mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa makundi maalum kushiriki katika ununuzi wa umma, lakini pia yanaibua suala la upatikanaji wa fursa hizo kwa usawa na uwezo wa wanufaika kutekeleza mikataba waliyopewa.

PPRA imeendelea kuhamasisha vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kujisajili katika mifumo rasmi ya ununuzi wa umma na kufuatilia zabuni zinazotangazwa na taasisi nunuzi.

Related articles

Recent articles