LAGOS, Nigeria
UTAFITI uliohusisha wanafunzi 222 kutoka vyuo vikuu 34 nchini Nigeria umebaini kuwa asilimia 52.1 hawajajiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao [2027].
Aidha, katika utafiti huo wa Campus Reporter, asilimia 31 walisema kukosekana kwa uwazi katika chaguzi na idadi ndogo ya wenzao kwenye siasa imechagia vijana wengi kutojihusisha na chaguzi.
Emmanuella Balogun, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Kwara (KWASU), ametimiza umri wa miaka 18 mwaka huu lakini hajajiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, akisema haamini utendaji kazi wa Tume ya Uchaguzi.
Mbali na kuona tume haiku huru, pia Emmanuella amepoteza imani na mchakato huo wa kidemokrasia baada ya kushuhudia mara kadhaa vitendo vya rushwa katika chaguzi zilizopita.
Kwa upande wake, Nurudeen Akewushola, ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe wa Nigeria, anasema vurugu katika uchaguzi wa mwaka 2023 zimechagia vijana wengi ‘kupuuzia’ kutokuona umuhimu wa kuacha mambo yao na kwenda kupiga kura.
Pia, baadhi ya vijana, akiwamo Kemisola Aboluwade, anasema aliacha kupiga kura baada ya kuona viongozi wanaoingia madarakani ni wale wale wasiotimiza yale waliyoahidi wakati wa kampeni.
“Inasikitisha zaidi, kwamba mwaka hadi mwaka, mambo yanazidi kuwa mabaya kwa sababu matarajio [ya wananchi] hayafikiwi,” amesema Aboluwade.
Katika Uchaguzi uliopita, 2023, wananchi wa Nigeria walikuwa na matumaini makubwa baada ya Tume ya Uchaguzi [INEC] kutambulisha mifumo ya teknolojia, ukiwamo wa kuonesha matokeo mubashara kwa idadi kura zilivyoendelea zikipigwa [IReV].
Kilichowashagaza wengi na kikitajwa pia kuchagia vijana wengi ‘kususia’ Uchaguzi wa 2027, mfumo huo ulichelewa kwa saa kadhaa baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.
Pia, zilikuwapo kasoro zingine, zikiwamo vurugu, kuchelewa kwa muda na vifaa vya kupigia kura katika baadhi ya vituo.
Ni kutokana na changamoto hizo na zingine, idadi ya wapigaji kura nchini Nigeria imeshuhudiwa ikiendelea kupungua kutoka uchaguzi mmoja na mwingine.
Mathalan, katika uchaguzi wa mwaka 2011, waliopiga kura ni asilimia 53.7 lakini idadi hiyo ilipungua hadi asilimia 43.7 mwaka 2015, kisha asilimia 34.75 mwaka 2019.
Katika Uchaguzi wa mwaka 2023, licha ya idadi ya waliojiandikisha kufikia milioni 87, ni asilimia 27 pekee waliojitokeza vituoni siku ya kupiga kura. Ni idadi ndogo zaidi kuwahi kutokea ndani ya miaka zaidi ya 40 ya hivi karibuni.
Anguko hilo linachangiwa na uamuzi wa vijana ‘kususia’ mchakato huo wa kidemokrasia. Ikumbukwe, vijana wa Nigeria wenye umri kati ya miaka 18 hadi 34 ndilo kundi kubwa zaidi, sawa na asilimia 40 ya raia wote wa nchi hiyo.


